KESI ya jinai ya kubaka na kumwingilia kinyume cha maumbile mkazi wa Yombo Dovya jijini Dar es saalam (jina limehifadhiwa), inatarajiwa kutolewa hukumu leo na Mahakama ya Hakimu Mkazi Dodoma.
Kesi hiyo Namba 23476 ya Mwaka 2024 inawakabili washtakiwa wanne wakiwamo askari wa Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ), MT 140105, Clinton Damas, askari magereza C.1693 Praygod Mushi, Nickson Jackson na Amin Lema.
Akizungumza na waandishi wa habari Septemba 27 mwaka huu, wakili wa washtakiwa hao, Meshack Ngamando alisema kila kitu kilichotakiwa kwenye kesi hiyo kimekamilika, kinachosubiriwa sasa ni uamuzi wa mahakama.
Alisema mwishoni mwa wiki walifanya mawasilisho ya mwisho ya kisheria kuhusu mwenendo wa kesi hiyo na kwamba wamewasilisha hoja kuhusu kasoro zilizojitokeza wakati wa usikilizaji.
"Tumepata nafasi ya kuwasilisha mawasilisho ya mwisho, kuhusu mwenendo wote wa kesi kuanzia hati ya mashtaka, ukamataji, utambuzi, mashahidi, vielelezo vilivyotolewa mahakamani kwa muda wa saa tatu na upande wa serikali nao umewasilisha yao kuanzia saa 11.00 jioni hadi saa moja usiku kwa hiyo kinachosubiriwa kwa sasa ni uamuzi wa mahakama," alisema Ngamando.
Alisema mwenendo wa kesi ulikuwa mzuri na kumbukumbu zilichukuliwa vizuri.
Wakili Godfrey Wasonga alisema wapo tayari kwa uamuzi utakaotolewa na mahakama.
Utetezi wa washtakiwa hao ulifungwa Septemba 26, 2024 ambao ulitolewa na washtakiwa pekee na hakukuwa na kielelezo chochote.
© 2025 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED