Waandishi wa IPP wang’ara tena tuzo umahiri wa uandishi habari

By Mwandishi Wetu , Nipashe
Published at 10:24 AM Sep 30 2024
Mhariri Mtendaji wa gazeti Nipashe, Beatrice Bandawe (wa tatu kulia), akifurahia jambo na waandishi wa habari wa IPP Media walioshinda Tuzo za EJAT 2023, jijini Dar es Salaam juzi. Kutoka kushoto Halfani Chusi (Nipashe), Christina Mwakangale (Nipashe)...
Picha:Mpigapicha Wetu
Mhariri Mtendaji wa gazeti Nipashe, Beatrice Bandawe (wa tatu kulia), akifurahia jambo na waandishi wa habari wa IPP Media walioshinda Tuzo za EJAT 2023, jijini Dar es Salaam juzi. Kutoka kushoto Halfani Chusi (Nipashe), Christina Mwakangale (Nipashe)...

WAANDISHI wa habari saba kutoka kampuni za IPP Media wametambuliwa na kutunukiwa Tuzo za Umahiri wa Uandishi wa Habari Tanzania (EJAT) wakati wa hafla ya utuzaji tuzo hizo iliyoandaliwa na Baraza la Habari Tanzania (MCT) jijini Dar es Salaam.

Katika hafla hiyo iliyofanyika juzi, Msanifu Mkuu wa gazeti Nipashe, Sanula Athanas aliibuka mshindi katika kipengele cha Habari za Elimu ambacho alishinda nafasi ya kwanza na ya pili upande wa magazeti.

Ripoti maalum kuhusu shule za nyasi wilayani Tunduru, mkoani Ruvuma iliyoripotiwa na gazeti hili Novemba mwaka jana ndiyo iliyotambuliwa na majaji wa tuzo hizo kuwa habari bora zaidi ya elimu kwa mwaka 2023 upande wa magazeti, ikifuatiwa na ripoti kuhusu 'Wilaya ya Bunda na maisha hasi kwa watoto' iliyochapishwa na Nipashe mwezi huo huo mwaka jana.   

Sanula, ambaye alikuwa Mshindi wa Jumla wa EJAT 2022, pia alitangazwa mshindi katika kipengele cha Kundi la Wazi, ambacho pia alishika nafasi ya kwanza na ya pili upande wa magazeti.

Ripoti ya uchunguzi kuhusu mkasa wa mjamzito kubakwa na hatimaye kufungwa katika kiroba wilayani Mkuranga, mkoani Pwani mnamo Juni 5 mwaka jana, ndiyo iliyotambuliwa na majaji wa EJAT 2023 kuwa habari bora zaidi kwa mwaka huo upande wa magazeti katika kundi hilo, ikifuatwa na ripoti nyingine ya Sanula kuhusu 'Maisha mapya ya wananchi wa Ukerewe, makazi na mashamba yakimezwa na ziwa'.

Sanula pia alipenya katika orodha ya waandishi wa habari watatu ya kumsaka Mshindi wa Jumla wa EJAT 2023, ikiwa ni mara ya nne mfululizo, akiingia katika kinyang'anyiro hicho kuanzia mwaka 2020.

Mwandishi wa habari wa Nipashe mkoani Dar es Salaam, Halfani Chusi, aliibuka mshindi katika kipengele cha Habari za Haki za Binadamu na Utawala Bora kutokana na ripoti yake ya uchunguzi kuhusu mkasa wa 'Askari-pori kudhuru wananchi Mbarali' kutokana na mgogoro wa kimpaka kati ya wanakijiji na Hifadhi ya Taifa Ruaha.   

Christina Mwakangale, mwandishi mwingine wa Nipashe mkoani Dar es Salaam, alishika nafasi ya pili katika kipengele cha Mwandishi Bora wa Habari za Ulinzi wa Vyanzo vya Maji na Mazingira.

Ripoti kuhusu hali ya dampo la Pugu, jijini Dar es Salaam, ndiyo imembeba Christina kushinda tuzo hiyo upande wa magazeti.

Saimon Rogers na Benjamin Mzinga, wote wa ITV, waliibuka washindi katika kipengele cha Haki za Binadamu na Utawala Bora kwa upande wa luninga, wakishirikiana kuandaa ripoti maalum kuhusu 'Watoto kula makombo ya mifupa ya nyama mnadani jijini Dodoma'.
Mshindi wa jumla wa tuzo hizo ni Mukrim Mohamed Khamis wa KTV TZ, akiweka rekodi kwa kuwa Mshindi wa Jumla wa kwanza kutoka Zanzibar katika historia ya tuzo hizo zilizotolewa kwa miaka 15 mfululizo.

Akizungumza wakati wa tuzo hizo, mgeni rasmi Naibu Waziri, Mussa Zungu, aliyemwakilisha Spika wa Bunge na Rais wa Umoja wa Mabunge Duniani (IPU), Dk. Tulia Ackson, alisema waandishi wa habari waendelee kujikita katika uandishi wa habari za weledi na usahihi, ili kuondoa migongano katika jamii na uvunjifu wa amani.

"Hakuna utafiti, hakuna haki ya kuongea. Uandishi ni zaidi ya upanga halisi, kalamu isipotumika vizuri inaweza kuvunja amani ya nchi. Waandishi mjikite katika ukweli hasa katika dunia ya sasa iliyokua kiteknolojia," alisema Zungu.

Pia aliwataka wadau wa habari nchini kuwasilisha serikalini sheria au vifungu vya sheria visivyokidhi matamanio ya waandishi wa habari ili vipelekwe bungeni kufanyiwa kazi.

"Bunge liko tayari kuweka mazingira wezeshi ili wanahabari kutekeleza majukumu yao kwa ufanisi. Serikali ni sikivu na Bunge litatenda haki, ili kukidhi matakwa ya wananchi, wanahabari ni sehemu yao.

"Bunge liko tayari kuboresha sheria ili kuwa na mazingira rafiki na wezeshi ili waandishi wa habari kufanya kazi zao kwa weledi," alisema.

Zungu pia aliwapongeza waandishi wa habari waliokidhi vigezo vya kuteuliwa kuwania tuzo hizo baada ya kupita katika mchujo wa jopo la majaji lililoongozwa na Halima Sharif.

Mwenyekiti wa Jopo la Majaji wa EJAT 2023, Halima, alisema kuna changamoto kadhaa zilijitokeza wakati wa kuzifanyia uchambuzi habari zilizowasilishwa zinazofikia 1,135, ikiwa ni pamoja na kujikita zaidi na vyanzo vya mikutano ya waandishi wa habari.

"Habari nyingi zilikuwa zimetokana na ‘press conference’ alisema… miongoni mwa vigezo tulivyozingatia ni habari zilizo na vyanzo sahihi na mahususi. Ni vyema habari izingatie vyanzo vyenye usahihi," alisema Halima.

Mwenyekiti wa Kamati ya Maandalizi ya tuzo hizo, Ernest Sungura, alisema kuna ongezeko la kazi zilizowasilishwa mwaka 2023 zilizofikia 1,135 kutoka kazi 893 za EJAT 2022.

Sungura ambaye pia ni Katibu Mtendaji wa MCT, alisema kazi za EJAT mwaka 2020 zilikuwa 396 na EJAT 2021 zilikuwa 608.

Alisema kuwa katika kazi za EJAT 2023, waandishi wa habari wa Mkoa wa Dar es Salaam wameongoza kwa kuwasilisha kazi 290, wakifuatiwa na Arusha (81), Mwanza (74) huku Iringa ikishika nafasi ya nne kwa kuwa na kazi 72.

Mkoa wa Mtwara ulishika nafasi ya tano kwa kuwa na kazi 49 huku kwa upande wa Zanzibar, kazi zilizopokewa ni kutoka Kaskazini Pemba (36) Pemba Kusini (43) na Mjini Magharibi (29).

Kati ya waandishi 72 walioshiriki kinyang'anyiro juzi, walituzwa tuzo za umahairi katika uandishi wa habari, wakijumuisha wanaume 45, sawa na asilimia 62.5 na wanawake ni 27 sawa na asilimia 37.5.

Sungura alisema kuwa kati ya wateule hao, 14 walitoka katika runinga, 13 vyombo vya mtandaoni, redio 20 na wateule 25 walitoka kwenye magazeti.