Polisi Tanzania yalala tena nyumbani

By Mwandishi Wetu , Nipashe
Published at 09:38 AM Sep 30 2024
Timu ya Polisi Tanzania.
Picha: Mtandao
Timu ya Polisi Tanzania.

TIMU ya Polisi Tanzania imeendelea kupoteza mechi zake za Ligi ya Championship, ikicheza uwanja wake wa nyumbani wa Ushirika mjini Moshi, baada ya juzi kuchapwa bao 1-0 dhidi ya TMA.

Timu hiyo iliyoshuka daraja msimu wa 2022/23, ilipoteza mchezo wake wa kwanza wiki iliyopita kwenye uwanja huo huo ilipofungwa bao 1-0 dhidi ya Mbuni FC.

Matokeo hayo yanaifanya kuwa kwenye nafasi ya 15, ikiwa haina bao wala pointi.

Bao la wageni katika mchezo huo liliwekwa wavuni na Abdulaziz Shahame, dakika ya 52 na kuipeleka hadi nafasi ya tano ya msimamo.

Wakati maafande wa Polisi wakisuasua, Biashara United imepata ushindi wake wa pili ikicheza uwanja wake wa nyumbani, Karume, Musoma mkoani Mara.

Bao pekee lililofungwa na Januari Benson, limeifanya timu hiyo kujizolea pointi zote tatu na kufikisha jumla ya pointi sita, baada ya wiki iliyopita kupata ushindi kama huo dhidi ya Transit Camp.

Kwa ushindi huo, Biashara inashika nafasi ya tatu ya msimamo, ikiwa na pointi sita na mabao sita, katika ligi hiyo ambayo inaongozwa na Mtibwa Sugar ambayo Ijumaa ilipata ushindi wake wa pili kwa kuitwanga Cosmopolitan mabao 2-0.

Mechi nyingine ilichezwa Uwanja wa Higland, Morogoro, ambapo wenyeji, Green Warriors waliwakaribisha African Sports na kuwachapa bao 1-0.

Green Warriors ambao wiki iliyopita walipoteza kwa bao 2-0 dhidi ya Mtibwa Sugar, wanashika nafasi ya nane kwenye msimamo wa ligi hiyo.