TAKRIBANI Watanzania 132 watanufaika na program mpya ya mafunzo ya ubobezi katika fani ya matumizi sahihi ya nishati, inayolenga kuongeza idadi ya wataalamu katika sekta hiyo, ikiwa ni mkakati wa kuongeza ufanisi na kupunguza uhaba wa umeme nchini.
Programu hiyo ya miaka mitatu ambayo iko katika hatua ya pili ya utekelezaji, inafadhiliwa na Shirika la Umoja wa Mataifa la Mpango wa Maendeleo (UNDP), Umoja wa Ulaya (EU) na Taasisi ya Teknologia Dar es Salaam (DIT), pia itasaidia katika kupunguza matatizo yatakayotokana na mabadiliko ya tabianchi katika sekta ya nishati.
Akizungumza leo mkoani Dar es Salaam wakati wa uzinduzi wa program hiyo, Kamishna Msaidizi wa Maendeleo ya nishati Mhandisi Styden Rwebangila, amesema mahitaji ya umeme na mafuta yanazidi kuongezeka nchini, lakini bahati mbaya mpaka sasa hakuna mifumo ya kudhibiti matumizi sahihi katika nyanja hiyo.
Amesema program hiyo inalenga zaidi kuwawezesha wataalamu mbalimbali kuwa na ufahamu wa jinsi ya ufuatiliaji na udhibiti umeme kwa watumiaji wakubwa wa nishati ili waweze kujiridhisha kwamba uniti wanazowapatia wanazitumia kwa usahihi.
“Ili tuweze kudhibiti ni lazima tuwe na wataalamu wanaojua kufuatilia matumizi ya nishati na wawe wamethibitishwa, na baadae serikali itakuja na kanuni za jinsi ya kudhibiti matumizi ya umeme kwa watumiaji wakubwa, na tunachokitarajia kila taasisi na mashirika makubwa aweko ofisa nishati,” amesema Mhandisi Rwebangila.
Ameongeza kuwa wanahitaji kila mwaka wawe wanafanya tathimini ya matumizi yao ya nishati na yale maeneo yatakayobainika kwamba yanahitaji kuboreshwa yaweze kufanyiwa kazi, na kwamba walichokifanya jana ni mwazo wa kujenga ‘skills’ kwa watanzania ili watakapofikia hatua hiyo wawe tayari na wataalamu kwenye soko kwaajili ya kutoa huduma hiyo.
Aidha, ameeleza kuwa ni rahisi kuokoa megawati moja kuliko kuwekeza kwenye kuzalisha kiasi kama hicho, na wanachokifanya sasa ni kupunguza msukumo kwa serikali kuendelea kuwekeza kwa wingi kwenye kitu kitakachoenda kutumika kwa matumizi yasiyokuwa sahihi.
“Hakuna haja ya kutumia taa ya Wati 100 ambayo mwanga wake unaweza kuupata kwa ‘bulb’ ya Wati tano, pia kwanini utumie kiyoyozi kinachotumia unit tano za umeme kwa siku wakati kuna uwezekano wa kutumia inayokula unit moja, hivyo maarifa ya kujua wapi kwenye tatizo yanahitajika ili kufikia malengo,” amesema Mhandisi Rwebangila.
Pia ameeleza kuna watu wanalalamika kwamba gharama za umeme zimepanda sana na zinawarudisha nyuma katika uzalishaji pasipo kujua kuwa kuna sehemu anapoteza, na kwamba lengo ni kuhakikisha wanakuwa na mtaalamu wa kusimamia matumizi hayo.
Mtaalamu wa Miradi UNDP, Abasi Kitogo, amesema wamefanikiwa kutengeneza mkakati ambao utaelekeza kwa undani jinsi gani ya kufikia malengo makuu ya kufikia matumizi bora ya nishati, ikiwemo kujenga uwezo wa DIT katika kutoa mafunzo mbalimbali ya sekta hiyo.
“Hatua ya kwanza tulifanikiwa kupata wataalamu 20 ambao walifanya mtihani na kufaulu vizuri, programu hii ni ya kwanza Tanzania, ukizingatia uchumi na matumizi ya nishati yanakuwa, viwanda na majengo yanaongezeka, hivyo kuwa na wataalamu watakaosaidia kupunguza matumizi yasio sahihi, itasaidi kukuza uchumi wa nchi,” amesema Kitogo.
Mmoja wa wanufaika wa program hiyo, Sherida Magomele, ameahidi kuwa watatumia vizuri fursa hiyo na kwenda kusaidia kupunguza matumizi ya nishati ili umeme utakao okolewa ukatumike katika maeneo mengine ambako gridi ya taifa haijafika.
© 2025 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED