Wataalam waonya matumizi holela ya dawa

By Christina Mwakangale , Nipashe
Published at 04:25 PM Nov 09 2024
Dawa.
Picha:Mtandao
Dawa.

WATAALAMU wa maabara, wauguzi, wafamasia na madaktari, wametakiwa kuzingatia utaratibu wa utoaji wa dawa kwa wagonjwa, ili kuondoa athari za matumizi holela ya dawa, hasa aina ya antibiotiki.

Mkurugenzi wa Huduma Shirikishi katika Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH), Dk. Mbonea Yonazi, alisema hayo jana jijini Dar es Salaam, wakati akifunga mafunzo ya siku mbili ya wataalamu hao kutoka hospitali tisa nchini, baada ya mafunzo ya kusimamia matumizi sahihi ya dawa.

Alisema mafunzo hayo ni muhimu kwa wataalamu hao ambao moja kwa moja hutoa huduma kwa wagonjwa hususani dawa aina ya antibiotiki, akisema yasipokuwa na matumizi sahihi hugeuka kuwa sugu katika ugonjwa na kusambaza na bakteria.

“Mfano unakuta mtu akiumwa kikohozi akapewa dawa za siku saba au nane, zisipofanya kazi tunarudi katika uchunguzi. Baadaye unakuja kubaini sababu ni dawa zimeshajenga usugu. Vimelea vya ugonjwa vikiwa sugu, tiba yake ni changamoto,” alisema Dk. Yonazi.

Pia alisema mafunzo hayo yalilenga kutoa mbinu za kudhibiti maambukizi katika hospitali, akisema mgonjwa anapofika na ugonjwa aina moja na kulazwa hospitalini, atibiwe na kupona badala ya kuondoka na magonjwa mengine.

 Bingwa wa Maradhi ya Ndani kutoka Hospitali ya Mnazi Mmoja, Zanzibar, Dk. Salma Hashoul Nassor, alisema mbinu zilizotolewa katika mafunzo hayo, zitaboresha majukumu yao katika vituo na hospitali.

Washiriki wa mafunzo hayo, akiwamo Dk. Salma ambaye pia ni Mwenyekiti Kamati inayosimamia, Kudhibiti na Utumiaji Sahihi wa Dawa za Antibiotiki, alisema kutokana na ongezeko la upingamizi wa dawa utokanao na usugu wa dawa, elimu hiyo ni sahihi kwa sasa.

Mfamasia kutoka Hospitali ya Rufani ya Mkoa wa Kagera ya Bukoba, Tatu Ibrahimu, alisema kutokana na baadhi ya watu kuchukua uamuzi wa kununua dawa kiholela bila kufuata utaratibu, inasababisha vimelea vya magonjwa kuwa sugu.

Dk. Rukia Ibrahim kutoka Hospitali ya Rufani Mkoa wa Singida, Idara ya Watoto, alisema kwa mujibu wa takwimu za dunia, zinakadiria ifikapo mwaka 2050, usugu wa vimelea dhidi ya dawa itakuwa janga la dunia.