BUNGE limeelezwa kuwa serikali inatengeneza mfumo wa kidijitali utakaowawezesha wastaafu wanaolipwa na Hazina kujihakiki wenyewe kupitia simu zao za mkononi au kwa kutumia huduma za kibenki.
Naibu Waziri wa Fedha, Hamad Hassan Chande, aliyasema hayo jana bungeni alipokuwa akijibu swali la Mbunge wa Nachingwea (CCM), Amandus Chinguile, aliyetaka kujua kwanini serikali isiweke utaratibu wa wastaafu kuhakikiwa katika halmashauri au kata badala ya utaratibu wa sasa wa kuhakikiwa mkoani.
Alisema uhakiki wa wastaafu wanaolipwa na Hazina umekuwa ukifanyika katika ngazi ya halmashauri na hata hivyo, ili kupunguzia gharama za wastaafu kwenda kujihakiki na kuwaondolea usumbufu wa kusafiri umbali mrefu ili kupata huduma hiyo, serikali inatengeneza mfumo huo.
Chande alisema baada ya kukamilika kwa taratibu zote, wastaafu watapewa elimu ya namna ya kujihakiki wenyewe na watatangaziwa siku ya kuanza kujihakiki.
Katika swali la nyongeza, Mbunge huyo alisema kuna wastaafu wanaishi vijijini na ni mbali na makao makuu ya halmashauri na kuhoji, serikali haioni wakati inatengeneza mfumo huo kusogeza huduma kwa wastaafu kwa kutumia watendaji wa kata na vijiji kutokana na hali zao si nzuri.
“Je, ni mshahara gani hutumika kutengeneza pensheni za wastaafu,” alihoji.
Naibu Waziri Chande alisema serikali imepokea ushauri wa Mbunge na itakwenda kufanyia kazi na kwamba, mshahara wa mwisho katika utumishi ndio hutumika kutengeneza pensheni kwa mstaafu.
© 2024 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED