Wanaswa na shaba zinazodaiwa za SGR

By Augusta Njoji , Nipashe
Published at 11:11 AM Nov 12 2024
Treni ya SGR.
Picha: Mtandao
Treni ya SGR.

JESHI la Polisi Mkoa wa Dodoma linawashikilia watu sita kwa tuhuma za kuharibu na kuiba nyaya za shaba katika mradi wa reli ya kisasa (SGR) maeneo ya wilaya za Mpwapwa na Bahi.

Akizungumza jana na waandishi wa habari jijini hapa, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Dodoma, George Katabazi, alisema kuwa katika wilaya ya Mpwapwa, jeshi hilo linawashikilia watu wawili; Said Sempinga (39) na Michael Robert (44), wote wakazi wa Kilosa kwa tuhuma za kuharibu miundombinu hiyo ya SGR.

Alisema tukio hilo lilitokea Oktoba 3 mwaka huu saa tano usiku katika kijiji cha Msagali, wilayani Mpwapwa ambako watuhumiwa wanadaiwa kukata na kuiba nyaya kwenye madaraja matatu ya reli hiyo.

"Kufuatia tukio hilo jeshi la polisi lilipata taarifa na kuanza uchunguzi wa tukio hilo mara moja kwa kushirikiana na wananchi na kufanikiwa kuwakamata watuhumiwa hao kwa nyakati tofauti wakiwa na nyaya hizo walizoiba kutoka kwenye reli ya umeme, uchunguzi unakamilishwa ili hatua zingine za kisheria zifuate," alisema.

Kamanda Katabazi alisema katika tukio lingine lililotokea Oktoba 8 mwaka huu maeneo ya Bahi sokoni, wilayani Bahi, walikamatwa watuhumiwa wanne kwa nyakati tofauti kwa tuhuma za kuhujumu miundombinu hiyo.

Aliwataja watuhumiwa hao kuwa ni Said Kapambwe (38), Petro Yassi (22), Michael Leyaseki (27) na Issa Misami (42).

Alitoa wito kwa wananchi kuendelea kushirikiana na polisi kutoa taarifa za uhalifu na wahalifu wanaohujumu miundombinu hiyo kwa kuwa wanaliingizia taifa hasara kubwa.