Wananchi wafunga barabara kushinikiza tembo kuondolewa

By Thobias Mwanakatwe , Nipashe
Published at 10:14 AM Oct 28 2024
Tembo.
Picha:Mtandao
Tembo.

WANANCHI wa Kijiji cha Mkiwa, wilayani Ikungi, mkoani Singida, wamefunga barabara kuu ya Dodoma - Singida kwa magogo ya miti kwa zaidi ya saa mbili, wakishiniza serikali ichukue hatua za kuwaondoa tembo waliovamia eneo hilo na kubomoa nyumba na kula mazao.

Wakizungumza na Nipashe jana eneo la tukio, baadhi ya wananchi hao walisema kundi la tembo hao lilivamia makazi yao juzi saa 10 jioni na kubomoa nyumba zao na kula vyakula, hali iliyoleta taharuki kubwa kijijini, wakazi wakikimbia ovyo. 

Ramadhani Ally, mmoja wa wakazi wa kijiji hicho, alisema tembo hao wameharibu miti na shamba la mihogo na kubomoa nyumba yake. 

Halima Shaban, mkazi mwingine wa kijiji hicho, alisema wameamua kufunga barabara hiyo, kushinikiza serikali ichukue hatua kwa kuwa mara kadhaa tembo wamekuwa wanavamia kijiji hicho na kufanya uharibifu wa nyumba na mashamba. 

"Tembo wamekuwa wakivamia makazi na hakuna kinachofanywa na serikali kuwadhibiti, kila mara tembo hawa wanatuharibia vitu na kutuacha masikini, sasa tumechoka," alitamka kwa hasira. 

Mbunge wa Singida Mashariki, Miraji Mtaturu na Mkuu wa Wilaya ya Ikungi, Thomas Apson, walifika eneo la tukio kuwatuliza wananchi hao ambao kutokana na kufunga barabara hiyo, walisababisha msongamano mkubwa wa magari na kuleta usumbufu kwa abiria. 

Mtaturu aliwaeleza wananchi hao kuwa kijiji na kata nzima ya Mkiwa na Isuna ni mapito ya tembo, hivyo inakuwa ngumu kuwazuia na kwamba serikali imekuwa inachukua hatua kuwadhibiti.

"Maliasili tunazihitaji na wanadamu tunawahitaji, niwaombe jitihada zinafanywa na serikali, hakuna makusudi yanafanyika katika kushughulikia suala hili. 

"Nitampigia simu Waziri wa Maliasili na Utalii (Balozi Dk. Pindi Chana), muda huu, ili aje yeye au awatume wawakilishi kuja kushughulikia suala hilo," alisema. 

Awali, mbunge huyo pia alimweleza Waziri wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Jerry Silaa, kwenye kikao cha majumuisho ya ziara yake ya siku tano mkoani Singida, kwamba tembo hao wamevamia makazi katika vijiji vya kata za Mkiwa na Isuna. 

Mara kadhaa tembo wamekuwa wanasababisha uharibifu wa mashamba na wakati mwingine kusababisha vifo kwa wananchi katika wilaya ya Ikungi, ambako makundi ya tembo yamekuwa yakipita kuelekea pori la akiba la Ruangwa lililoko Itigi, wilayani Manyoni.

Ni ishara ya kuwapo uvamizi katika shoroba za wanyamapori nchini.  

Ndovu huwa hawasahau eneo ambako wao wenyewe walipita zamani, watangulizi (wazazi au ukoo wao) walipita awali, hata kama ni miaka 1,000 imepita.