Wafunga barabara kupinga mfumo stakabadhi ghalani

By Thobias Mwanakatwe , Nipashe
Published at 10:16 AM Sep 09 2024
Wafanyabiashara wa mazao na makuli mkoani Singida wakiwa wamefunga barabara kuu ya Dodoma-Singida-Mwanza juzi eneo la uwanja wa mpira wa Liti mjini Singida wakipinga Mfumo wa Stakabadhi ghalani.
PICHA: THOBIAS MWANAKATWE
Wafanyabiashara wa mazao na makuli mkoani Singida wakiwa wamefunga barabara kuu ya Dodoma-Singida-Mwanza juzi eneo la uwanja wa mpira wa Liti mjini Singida wakipinga Mfumo wa Stakabadhi ghalani.

WAFANYABIASHARA wa mazao na wabeba mizigo mjini Singida wameandamana na kufunga barabara kuu ya Dodoma-Singida-Shinyanga kwa magogo na miti wakipinga mfumo wa stakabadhi ghalani.

Maandamano hayo yalifanywa juzi, wakifunga barabara kwa muda wa saa moja katika eneo la Uwanja wa Liti baada ya kukamatwa magari yao ambayo yalikuwa yamebeba mazao waliyonunua kutoka vijijini; kwamba serikali ilitaka wakayauze kwa mfumo huo.

Hata hivyo, askari wa Jeshi la Polisi mkoani Singida walifika katika eneo hilo na kuwatawanya wafanyabiashara hao na kufungua barabara hiyo.

Wakizungumza na Nipashe, wafanyabiashara hao, akiwamo Abubakari Francis, walisema mfumo wa stakabadhi ghalani ni mzuri, lakini una upungufu kwa sababu wananchi hawajapewa elimu ya namna ya kuuza mazao yao.

Mfanyabiashara Mohamed Nassoro alisema utaratibu wa kuuza mazao kwa kutumia mfumo huo usitishwe kwanza msimu huu, ili serikali itoe elimu kwa wananchi.

Mkuu wa Mkoa wa Singida, Halima Dendego, alifika eneo hilo na kueleza kuwa uuzaji mazao kwa kutumia mfumo wa stakabadhi ghalani umeleta mapinduzi makubwa katika biashara ya mazao mkoani mwake.

Akitoa mfano, Halima alisema bei ya dengu imepanda hadi kufikia Sh. 2,060 kwa kilo na kwamba utaratibu huo umepunguza changamoto zilizokuwa zinawakumba wakulima kama vile upotevu wa mazao, bei duni na unyonyaji kutoka kwa wafanyabiashara.

Halima alisema: "Kumekuwa na ongezeko la bei ya dengu ambapo awali zilikuwa zinauzwa kati ya Sh. 900 na1,300 kwa kilo. Katika msimu wa 2023/24 na sasa inauzwa kati ya Sh. 1,670 na 2,060 kwa kilo."

Alisema kuwa kutokana na mafakikio hayo, serikali mkoani Singida itaendelea kuhamasisha wakulima kutumia mfumo huo kwa faida ya maendeleo ya kilimo na uchumi wa taifa.

Alisema pamoja na mafanikio katika kutumia mfumo huo, kumekuwa na changamoto kadhaa kutokana na baadhi ya wafanyabiashara kutokubaliana na mfumo huo kwa madai hawapati faida kubwa ambayo walikuwa wanapata awali.

Halima alisema kuwa kutokana na kuongezeka kwa bei ya dengu, mapato ya halmashauri pia yameongezeka, wamedhibiti utoroshaji mazao hali iliyowezesha serikali kuwa na uhakika wa takwimu, urahisi wa mikopo kwa wakulima na kuongezeka kwa masoko ya uhakika ya ndani na nje ya nchi.

Mkoa wa Singida ulizindua rasmi utekelezaji wa mfumo wa stakabadhi ghalani kwa msimu 2024/25 kufuatia maagizo yaliyotolewa na serikali kupitia mwongozo wa biashara ya dengu, mbaazi na ufuta.

Mwongozo huo ulitolewa chini ya usimamizi wa Mamlaka ya Udhibiti wa Nafaka na Mazao Mchanganyiko (COPRA), Tume ya Maendeleo ya Ushirika (TCDC), Bodi ya Usimamizi wa Stakabadhi za Ghala (WRRB) na Soko la Bidhaa (TMX).