Wachanga Mil 2.9/- kujenga sekondari ya kijiji chao kumuenzi Prof. Massamba

By Sabato Kasika , Nipashe
Published at 02:24 PM Mar 28 2024
Baadhi ya wakazi wa Kijiji cha Kurwaki wakiwa katika picha na mbunge Prof. Sospeter Muhongo (katikati mwenye tisheti nyeupe), baada ya mbunge kukabidhi mifuko ya saruji.
Picha: Mpigapicha Wetu
Baadhi ya wakazi wa Kijiji cha Kurwaki wakiwa katika picha na mbunge Prof. Sospeter Muhongo (katikati mwenye tisheti nyeupe), baada ya mbunge kukabidhi mifuko ya saruji.

WAKAZI wa Kijiji cha Kurwaki, Kata ya Mugango Musoma Vijijini mkoani Mara, wameanza ujenzi wa Shule ya Sekondari David Massamba Memorial ili kumuenzi bingwa huyo wa Kiswahili.

Sekondari hiyo  itakuwa ya pili kwa Kata ya Mugango, imepewa jina  jina la marehemu Prof. David  Massamba, ambaye alikuwa mzaliwa wa kijiji hicho  aliyekuwa bingwa lugha ya Kiswahili.

Michango ya awali ya ujenzi kutoka kwa wakazi wa kijiji hicho ni Sh. 1,870,000, familia Prof. Massamba Sh. 800,000, mchango wa wazaliwa wa Kurwaki wanaoishi maeneo mengine ni Sh. 750,000.

Kwa mujibu wa mbunge wa Musoma Vijijini, Profesa Sospeter Muhongo, wadau wengine waliochangia ujenzi huo ni diwani wa Kata ya Mugango Sh.200,000, wakazi wa kijiji jirani cha Kiriba Sh.  80,000, walimu na makada wa CCM Sh. 70,000

Amesema, yeye amechangia mifuko 250 ya saruji, mfuko wa jimbo umechangia mifuko 205 ya saruji, na kwamba michango zaidi inahitajika kupitia akaunti ya kijiji Benki ya NMB jina ni Kijiji cha Kurwaki.

"Tafadhali tunaomba tuendelee kuchangia ujenzi wa sekondari hii ambayo itakuwa ni kumbukumbu nzuri ya kuenzi kazi nyingi na muhimu alizozifanya Prof. Massamba kwenye ukuzaji na usitawishaji wa lugha ya Kiswahili kitaifa na kimataifa," Prof. Muhongo amesema.

Prof. Massamba alifariki dunia Agosti mwaka jana. Alikuwa bingwa wa mabingwa wa lugha ya Kiswahili aliyefanya kazi kubwa ya ustawishaji wa lugha ya Kiswahili kwa kushirikiana na wataalamu wenzake.

Miongoni mwa kazi alizofanya, ni kuandika vitabu vinavyotumika vyuo vikuu na sekondari (Sarufi Maumbo ya Kiswahili Sanifu), uandishi wa kamusi ya Kiswahili.