Serikali kujenga barabara Zilizoharibiwa na mvua

By Shaban Njia , Nipashe
Published at 02:51 PM Apr 28 2024
Wakazi wa Kata ya Ngaya Halmashauri ya Msalala, mkoani Shinyanga wakisukuma gari lenye namba za usajili T.334 ALW aina ya CANTER iliyokwama katika barabara ya Ngaya-Busangi.
Picha: Shaban Njia
Wakazi wa Kata ya Ngaya Halmashauri ya Msalala, mkoani Shinyanga wakisukuma gari lenye namba za usajili T.334 ALW aina ya CANTER iliyokwama katika barabara ya Ngaya-Busangi.

SERIKALI imesema barabara zote zilizoharibika kutokana na mvua zinazoendelea kunyesha sehemu mbalimbali nchini, zitarekebishwa mara baada ya mvua kuisha ili kurejesha mawasiliano kama ilivyokuwa hapo awali.

Hayo yamebainishwa na Mkuu wa Wilaya ya Kahama Mboni Mhita baada ya kushuhudia wakazi wa Kata ya Ngaya katika Halmashauri ya Msalala, wakisukuma gari lenye namba za usajili T.334 ALW aina ya Canter iliyokuwa imekwama katika barabara ya Ngaya-Busangi, ambayo imeharibika kutokana na mvua mvua hizo.

Mboni amesema, kutokana na mvua zinazoendelea kunyesha katika maeneo yote ya halmashauri za Msalala, Ushetu na Manispaa ya Kahama, miundombinu mingi ya barabara imeharibika.

“Hii siyo Kahama peke yake bali ni nchi nzima, naomba niwatoe hofu kuwa Serikali itarejesha miundombinu kama ilivyokuwa awali kabla ya mvua,” amesema.

Aidha, mkuu wa wilaya huyo alilazimika kupita kwenye barabara hiyo wakati akifanya ziara ya kukagua miradi mbalimbali ya maendeleo, ambapo aliwataka wakandarasi wanaoendelea na ujenzi wa miundombinu hiyo ili kuhakikisha zile barabara zilizokata mawasiliano baina ya kata hadi kata, kijiji mpaka kijiji zinarekebishwa.