TMA yapongezwa kwa kutoa taarifa sahihi za hali ya hewa

By Mwandishi Wetu , Nipashe
Published at 06:18 PM Apr 30 2024
Kaimu Mkurugenzi wa Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA), Dk Ladslaus Chang'a, akizungumza na Baraza la wafanyakazi wa mamlaka hiyo leo mkoani Morogoro.
PICHA: MPIGAPICHA WETU
Kaimu Mkurugenzi wa Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA), Dk Ladslaus Chang'a, akizungumza na Baraza la wafanyakazi wa mamlaka hiyo leo mkoani Morogoro.

WAFANYAKAZI wa Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA), wamekutana kwaajili ya kupitia kikao cha Baraza la Wafanyakazi wa TMA kilichofanyika katika ukumbi wa NSSF mkoani Morogoro kwa lengo la kufanya tathmini ya utendaji kazi wa Mamlaka kwa kuzingatia maazimio ya Baraza lililopita pamoja na kupitia bajeti ya mwaka 2024/2025. Baraza hilo lilifunguliwa rasmi na Mwenyekiti wa Bodi ya TMA, Jaji Mshibe Bakari.

Jaji Mshibe amewapongeza watumishi wote kwa kazi nzuri wanayoendelea kuifanya ya utoaji wa taarifa sahihi za hali ya hewa kwa wakati, taarifa ambazo zimesaidia wananchi na Taifa kwa ujumla kuchukua hatua stahiki. Pongezi hizo zilitolewa pia na Makamu Mwenyekiti wa Bodi ya TMA, Dk. Emmanuel Mpeta, viongozi wa TUGHE Taifa, Wizara na TMA.

 “Kwa namna ya pekee niendelee kuwapongeza Menejimenti na wafanyakazi wote wa TMA kwa kuendelea kutoa na kusambaza kwa wakati utabiri bora ambao unasaidia kuokoa maisha ya watu na mali zao, ambapo kwa mvua za vuli zilizoambatana na EL NINO kiwango cha usahihi wa utabiri kilikuwa asilimia 98”. amesema Jaji Mshibe.

Mwenyekiti wa Bodi ya Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA), Jaji Mshibe Ali Bakari, akizungumza na Baraza la wafanyakazi wa mamlaka hiyo leo mkoani Morogoro.
“Aidha, naendelea kuwakumbusha utendaji kazi wenye weledi na unaozingatia sheria na taratibu za kazi, sisi sote tukashirikiane kutimiza majukumu yetu ili kwenda sambamba na falsafa ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dk. Samia Suluhu Hassan ya “Kazi Iendelee”.” amesisitiza Jaji Mshibe.

 Awali, Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa TMA na Makamu Mwenyekiti wa Jopo la Kimataifa la Mabadiliko ya Sayansi ya Hali ya Hewa na Tabianchi, Dk. Ladislaus Chang’a ameeleza kuwa lengo la kikao hicho cha baraza ni kujadili na kupitisha mapendekezo ya bajeti ya mamlaka kwa mwaka wa fedha 2024/25 na kufanya tathmini ya utendaji wa mamlaka katika mwaka wa fedha 2023/2024.

Aidha, taarifa ya utendaji kwa kipindi cha mwaka wa fedha 2023/24 imeainisha kazi zilizotekelezwa katika kipindi tajwa, mafanikio yaliyopatikana, changamoto na mikakati  ya kutatua changamoto husika.