TANROADS yafikisha km 37,226 za barabara nchini

By Augusta Njoji , Nipashe
Published at 04:13 PM Feb 18 2025
Mkurugenzi wa Mipango ya Miundombinu wa wakala huo, Mhandisi Ephatar Mlavi
Picha: Mtandao
Mkurugenzi wa Mipango ya Miundombinu wa wakala huo, Mhandisi Ephatar Mlavi

WAKALA ya Barabara Tanzania (TANROADS), umesema ndani ya miaka minne ya uongozi wa Rais Samia Suluhu Hassan, hali ya barabara kuu na za mikoa zilizo katika hali nzuri na wastani imeimarika na kufikia asilimia 90 ya mtandao wote wa barabara wenye kilomita 37,225.72.

Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dodoma, Mkurugenzi wa Mipango ya Miundombinu wa wakala huo, Mhandisi Ephatar Mlavi, alisema alipoingia Rais Samia, hali hiyo ilikuwa kwa zaidi ya asilimia 80 na sasa imefikia 90.

Alisema kwa kipindi hicho yamepatikana mafanikio makubwa katika kuboresha miundombinu ya barabara, madaraja na viwanja vya ndege nchini, ikiwamo barabara zenye urefu wa jumla ya kilomita 15,625.55 zimekuwa katika hatua mabalimbali za utekelezaji.

Alifafanua kuwa barabara zenye urefu wa kilomita 1,365.87 zimekamilika kujengwa kwa kiwango cha lami na kilometa 2,031.11 zimeendelea kujengwa kwa kiwango cha lami, huku kilomita 2,052.94 na madaraja mawili zimefanyiwa upembuzi yakinifu na usanifu wa kina na serikali inatafuta fedha za kuzijenga kwa kiwango cha lami.Vilevile, alisema upembuzi yakinifu na usanifu wa kina wa barabara kilomita 4,734.43 na madaraja 10 unaendelea.

“Aidha, miradi ya barabara yenye urefu wa takriban kilomita 5,326.90 na miradi saba ya madaraja ipo katika hatua ya manunuzi, kwa ajili ya kufanyiwa upembuzi yakinifu na usanifu wa kina ikiwa ni maandalizi ya ujenzi na ukarabati wa barabara hizo kwa kiwango cha lami,” alisema.

Pia, alisema katika kipindi tajwa madaraja makubwa tisa yamekamilika kujengwa kwa gharama ya Sh. bilioni 381.301 ambayo ni Gerezani (Dsm); Daraja jipya la Tanzanite (Dsm); Wami (Pwani); Kitengule (Kagera); Kiyegeya (Morogoro); Ruaha (Morogoro); Ruhuhu (Ruvuma); Mpwapwa (Dodoma) na daraja la Msingi (Singida).

Hata hivyo, alisema madaraja 10 ambayo ni Kigongo – Busisi, Lower Mpiji, Mbambe, Simiyu, Pangani, Sukuma, Kerema Maziwani, Kibakwe, Mirumba na Jangwani ujenzi wake unaendelea kwa gharama ya Sh. bilioni 985.8.

Pamoja na hayo, alisema madaraja makubwa 19 yako kwenye maandalizi ya kujengwa ambayo ni: Godegode (Dodoma); Ugala (Katavi); Kamshango (Kagera); Bujonde (Mbeya); Bulome (Mbeya); Chakwale (Morogoro); Nguyami (Morogoro); Mkundi (Morogoro); Lower Malagarasi (Kigoma); Mtera (Dodoma); Kyabakoba (Kagera); Mjonga (Morogoro); Doma (Morogoro), Sanga (Songwe); Kalebe (Kagera), Ipyana (Mbeya); Mkondoa (Morogoro); Kilambo (Mtwara) na Chemchem (Singida).

UDHIBITI WA UZITO WA MAGARI

Alisema katika kupunguza foleni ya magari katika mizani zenye magari mengi, Wizara ya Ujenzi kupitia Tanroads, imefunga mizani 20 za kupima magari yakiwa kwenye mwendo katika Mikoa ya Pwani, Morogoro, Iringa, Songwe, Dodoma, Singida, Arusha na Mara.

Kuhusu ushiriki wa wazawa katika utekelezaji wa miradi, Mkurugenzi huyo alisema Makandarasi wazawa 1,036 walipata mikataba ya kazi ya zaidi ya Sh. bilioni 383.9, huku ushiriki wao katika miradi ya ujenzi wa Barabara Kuu na Barabara za Mikoa hauridhishi.

“Tanroads imeweka mpango maalum wa miaka mitano wa kukuza uwezo na ushiriki wa Wazawa katika kazi za ujenzi wa barabara na madaraja, ikiwamo kutenga asilimia 10 ya bajeti ya kila mwaka ya maendeleo kwa ajili ya Miradi ya mafunzo kwa vitendo kwa Makandarasi Wazawa ili kuwajengea uwezo,”alisema.

Alisema pia kutenga angalau asilimia 30 ya bajeti ya maendeleo, kwa ajili ya upendeleo kwa wazawa na angalau asilimia tano kwa ajili ya makundi maalum.

Kadhalika, alitoa ufafanuzi kuhusu msongamano wa Babarabara za Dar es salaam  na Pwani, zinazoendelea kupanuliwa kuwa kumekuwapo na njia za mchepuko huku barabara ya zamani ya Kibaha hadi Chalinze imeanza kufanyiwa matengenezo baadhi ya maeneo, ili ianze kutumika.

MIKAKATI MAALUM DODOMA

Alisema katika kukabiliana na msongamano wa magari Jiji la Dodoma, serikali imepanga kupanua barabara kwa kilometa 220 kwa njia nne zinazoingia kutokea Iringa(Km 50), Singida(Km 50), Dar es salaam (Km 70)na Arusha(Km 50).

“Ujenzi wa barabara ya mzunguko wa nje katika Jiji la Dodoma kwa kiwango cha lami yenye jumla ya urefu wa Kilometa 112, kwa lengo la kupunguza msongamano wa magari katikati ya Jiji. 

“Hadi kufikia Februari, 2025, ujenzi umefikia asilimia 91 kipande cha Nala – Veyula – Mtumba – Ihumwa Bandari Kavu (km 52.3) na asilimia 85 kwa kipande ya Ihumwa Bandari Kavu – Matumbulu – Nala (km 62).2