Sakata binti aliyebakwa lachukua sura mpya

By Jenifer Gilla , Nipashe
Published at 10:39 AM Aug 20 2024
Watuhumiwa wa ubakaji (kulia mwenye fulana nyekundu na madoa) wakiwa chini ya ulinzi wakisubiri kusomewa mashtaka yao katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Dodoma jana.
Picha: Mpigapicha Wetu
Watuhumiwa wa ubakaji (kulia mwenye fulana nyekundu na madoa) wakiwa chini ya ulinzi wakisubiri kusomewa mashtaka yao katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Dodoma jana.

SAKATA la binti anayedaiwa kuwa mkazi wa Yombo Dovya, Temeke mkoani Dar es Salaam, aliyebakwa na kulawitiwa na wanaodaiwa kuwa askari waliotumwa na bosi wao ‘Afande’, limechukua sura mpya.

Hatua hiyo ni baada ya mjadala mkali kuibuka katika mitandao ya kijamii kutokana na kauli iliyotolewa juzi na aliyekuwa Kamanda wa Polisi Mkoa wa Dodoma, Kamishna Msaidizi Mwandamizi (SACP) Theopista Mallya, alipohojiwa na gazeti la Mwananchi na kusema uchunguzi wa jeshi hilo umebaini kuwa binti huyo alikuwa anajiuza.

Hata hivyo, saa tano baada ya habari hiyo kusambaa, Mkuu wa Jeshi la Polisi nchini, Inspekta Jenerali (IGP) Camillus Wambura, alitangaza kumhamishia Kanamda Malya makao makuu ya jeshi hilo. 

Alisema pia jeshi hilo lilibaini vijana wanaotuhumiwa kumfanyia binti huyo kitendo hicho walikiri kutoagizwa na askari kama ilivyoelezwa na pia walikuwa walevi na wavuta bangi.

Baada ya taarifa hiyo kusambazwa kwenye mitandao ya kijamii iliibua hisia kali kwa wananchi ambao waliandika ujumbe wa kulilaumu jeshi hilo kwa kutomtendea haki binti huyo huku wakiamwambatanishia Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum, Dk. Dorothy Gwajima, na Waziri wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa, Dk. Stergomena Tax, wakiwataka waingilie kati.

Meya wa zamani wa Ubungo, Boniface Jacob, ambaye aliibua sakata hilo wiki mbili zilizopita, aliandika maelezo yenye ukurasa wake wa X akieleza masikitiko yake kuwa licha ya nchi kuwa na viongozi wakuu wanawake, haki ya binti huyo inachelewa kupatikana.

Alisema inasikitisha licha ya Kamanda wa Polisi Dodoma ambaye ni mama, kushiriki kuhukumu na kuharibu kesi ya mwanamke mwenzake kwa kusema maneno mabaya na ya uongo hadharani, ili binti akose msaada na kupoteza haki yake.

Jacob alisema binti huyo hakuwa anajiuza kama alivyosema kamanda bali anafahamika kwa mwenendo mzuri, aliyepaswa kuhitimu kidato cha nne mwaka huu kama si kukatisha masomo yake akiwa kidato cha pili baada ya kushindwa kuelewa masomo darasani na kuajiriwa kufanya kazi katika baa iliyoko Dodoma.

Alisema kauli hiyo, iliyokanushwa na jeshi hilo kuwa si ya taasisi, kwamba alikuwa anajiuza ilhali amefanyiwa kitendo cha kinyama, inamuumiza zaidi binti huyo na familia yake na  kutafsiri kama nia ovu ya  kupoteza haki yake.

“Ninatarajia kuona katika kesi hii wanawake wote Tanzania wanaungana kumtetea binti JM na kujakikisha haki inatendeka kama sehemu ya kulinda wanawake wengine dhidi ya ubakaji na udhalilishaji,” aliandika Jacob.

Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) Kanda ya Kaskazini, Godbless Lema, aliandika kwenye ukurasa wake wa Instagram kuwa alitegemea kuona kauli za polisi zikiwa zimejaa utu, haki na huruma kwa binti huyo kwani hata angekuwa kweli anajiuza hakustahili kufanyiwa vitendo hivyo vya ukatili.

“Mtoto wako angefanyiwa ukatili huu na video zake kusambazwa pengine kauli zenu zingejaa utu, haki na huruma , mtalipa kila dhambi mnayoitunza kwa maelekezo,” alisema.

Mmoja wa watumiaji wa mitandao hiyo, Carol Ndosi, aliandika kwenye ukurasa wake wa X kuwa kitendo alichofanyiwa binti huyo ni cha kinyama na wale wote wanaotengeneza mazingira ili waliohusika wasiwajibishwe ni wanyama zaidi.

Mtumiaji mwingine aliyejulikana kwa jina la Choki Junior, alihoji kwenye ukurasa wa Instagram  kuwa: “Hata awe anajiuza ni haki afanyiwe vile? Ukiangalia tu video unahisi aliridhia kufanyiwa vile kwa sababu ya pesa? Mvuta Bangi au mlevi yuko sahihi kumtendea mtu vile? Vaa viatu vya mzazi wa yule binti halafu polisi unaowategemea wanakuletea taarifa hivi, kichaa anachekesha sana kama hatoki kwenye familia yako.”

WAZIRI AINGILIA KATI

Kauli hizo zilimwibua Waziri Gwajima na kuandika kwenye ukurasa wake wa Instagram kuwa amepokea hisia, maoni na maswali ya wananchi na amewasiliana na Waziri wa Mambo ya Ndani, Hamad Masauni na anayafanyia kazi.

“…  ni dhahiri kuwa alichofanyiwa 'Binti wa Yombo' ni kitu kibaya kisicho cha utu hivyo, anastahili haki yake kwa mapana yote. Ndugu Wananchi, Nawasihi tujipe muda na kuamini kuwa, haki itatendeka kwa mujibu wa sheria na itaonekana bayana na siyo vinginevyo,” aliandika Waziri Gwajima. 

POLISI YAOMBA RADHI

Baada  ya taarifa hiyo kusambaa, polisi waliibuka na  kutoa taarifa ya kuomba radhi kwa Watanzania na kumhamisha Kamanda Theodora kituo cha kazi wakati uchunguzi wa usahihi wa kauli aliyoitoa ukiendelea.

Taarifa iliyotolewa Msemaji wa Jeshi la Polisi, Naibu kamishna (DCP) David Misime, jana ilisema kauli iliyotolewa si ya jeshi hilo bali ya mtu binafsi na kuwa kauli sahihi ni zile alizozitoa kwa umma Agosti 4,6 na 9, mwaka huu, na watuhumiwa walifikishwa mahakamani jana.

“Jeshi la Polisi lingependa kuomba radhi kwa kila mmoja aliyeguswa na kuchukizwa na kauli hiyo inayosambaa kwenye vyombo vya habari wakati ufutiliaji ukifanyika kupata usahihi wake.

“Wakati uchunguzi  wa kupata usahihi wa kauli hizo ukiendelea, Mkuu wa Jeshi la Polisi amefanya mabadiliko madogo kwa kumhamisha Kamanda Theopista Mallya kwenda Makao Makuu ya Polisi Dodoma na nafasi yake kuchukuliwa na Kamishna Msaidizi Mwandamizi (SACP)  George Katabazi,” alisema Misime.

WABUNGE WANAWAKE

Nao wabunge wanawake wamelipongeza Jeshi la Polisi na Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi kwa hatua za awali za kumwondoa Kamanda Mallya. 

“Tunataka haki itendeke kwa binti aliyebakwa na kulawitiwa na wahusika wote wafikishwe mahakamani haraka akiwamo anayetuhumiwa kuwatuma kubaka na kulawiti,” lilisema tamko hilo.

LHRC YAIBUKA 

Jana Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC), kilitoa taarifa kwa umma kuwa kuna maswali 11 kwenye taarifa zinazotolewa na polisi. 

Mkurugenzi Mtendaji wa LHRC, Dk. Anna Henga, aliuliza maswali hayo kuwa ni taarifa zipi ni sahihi kutoka Jeshi la Polisi Makao Makuu, Wizara Mambo ya Ndani au Makamanda wa Polisi wa Kanda Maalum ya Dar es Salaam na Dodoma? Je, watuhumiwa ni maofisa wa jeshi lipi?” 

Maswali mengine ni watuhumiwa katika tukio hilo walikuwa watano, je huyo mwingine ni nani na yuko wapi? binti alilazimishwa kumuomba msamaha ‘Afande’, je Afande ni nani? Je Mhanga (mwathirika) yuko salama katika mikono ya wanaomhumkumu kuwa ni kama alikuwa anajiuza?” 

Je, Binti huyo kuwa katika mikono ya Polisi hakutaathiri upatikanaji wa haki na ushahidi? Je, mtu kuwa kama anajiuza inahalalisha kufanyiwa vitendo vya ukatili ikiwepo kubakwa?, Je kwa vitendo hivi Jeshi la Polisi linasimamia maslahi ya nani?” 

Je kuwa mlevi na mvuta bangi ni kinga dhidi ya uhalifu?, Kwa kutajwa Afande bila kusema ni afande wa jeshi gani je Polisi hawana mgogoro wa maslahi na hili shauri?  Na taarifa ya Polisi ya August 9 2024 ilisema upelelezi umekamilika na leo ni tarehe 19, je ni lini shauri hili litapelekwa Mahakamani?” 

“LHRC inapenda kuwakumbusha kuwa kitendo alichofanyiwa muhanga ni cha kinyama, kikatili, kinyume na haki za binadamu na sheria za Nchi na kwamba yeyote atakayefumbia macho vitendo hivyo ni adui wa haki na utu, LHRC inapenda kutoa wito kwa Jeshi la Polisi kuacha kulinda na kutetea uhalifu kwani kauli ya RPC Dodoma ni wazi inatetea wahalifu na uhalifu uliofanyika,” alisema Henga.  

“Pia Polisi itoe nafasi kwa Binti Muhusika kupata huduma ikiwepo ya ushauri nasihi kutoka kwa chombo ambacho hakina maslahi na shauri hili,” aliongeza. 

…Watuhumiwa ubakaji, ulawiti wafikishwa mahakamani

 

Renatha Msungu na Paul Mabeja, DODOMA

WATU wanne wanaotuhumiwa kutumwa na askari kumlawiti na kumbaka binti mkazi wa Yombo Dovya, jijini Dar es Saalam, jana walifikishwa Mahakama ya Hakimu Mkazi Mkoa wa Dodoma na kusomewa mashtaka mawili.

Watuhumiwa hao walifikishwa mchana katika mahakama hiyo na kusomewa mashtaka ya kubaka kwa kikundi (gang rape) na kumwingilia kinyume na maumbile binti huyo.

Washtakiwa hao wametajwa kuwa ni Clinton Damas, Askari wa Jeshi la Wananchi Tanzania (JWTZ), Amin Lema, Nickson Jackson na Praygod Mushi ambaye ni Askari wa Jeshi la Magereza.

Washtakiwa hao walifikishwa mahakamani wakiwa chini ya ulinzi wa polisi, mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu wa Mahakama hiyo, Zabibu Mpangule.

Ilidaiwa mahakamani hapo ya kuwa washtakiwa hao walitenda makosa hayo kati ya Mei 25 na Mei 26, mwaka huu.

Hata hivyo, washtakiwa hao walikana mashtaka na kesi hiyo imepangwa kuanza kusikilizwa leo mchana.

Akizungumza nje ya mahakama Mkurugenzi Msaidizi Ofisi ya Taifa ya Mashtaka Makao Makuu, Renatus Mkude, alisema kuwa mahakama imetoa amri ya kumlinda binti aliyefanyiwa ukatili kwa jina lake kufichwa ili asipate fedheha na kudhalilika.

“Na washtakiwa wamenyimwa dhamana kwa sababu za kiusalama na wataendelea kubaki rumande," alisema.

Alisema kuwa kesi hiyo ambayo upelelezi wake umekamilika itaanza kusikilizwa mfululizo kuanzia leo hadi Ijumaa wiki hii.

Hata hivyo, aliitaka jamii kuwa na utulivu wakati sheria inachukua mkondo wake.

"Tunaamini haki itatendeka kadiri sheria inavyotaka, Ofisi ya Taifa ya Mashtaka itahakikisha haki inatendeka," alisema.

Katika hali ambayo haikutarajiwa waandishi wa habari walizuiwa kuingia kwenye chumba maalum ambacho watuhumiwa hao walifikishwa mbele ya hakimu, na kulazimika kupata maelezo ya kesi kwa wanasheria na hakimu.