Bodi ya Maji ya Bonde la Wami/Ruvu, Kidakio cha Pwani, Mamlaka ya Usimamizi wa Mazingira (NEMC), kwa kushirikiana na Halmashauri za Manispaa za Ubungo na Kinondoni wamepanda miti 5,000 ya Michikichi katika bonde la Mto Mpiji.
Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Albert Chalamila ndiye aliyezindua programu hiyo kwa kupanda mche mmoja wa zao hilo ambalo mbali na kutunza mazingira lakini linafaida kwa wakazi wanaoishi karibu na bonde hilo.
Kauli mbiu ya mradi huo “Michikichi kwa Uhifadhi wa Mazingira na Uchumi Endelevu,” unalenga kuleta mabadiliko ya muda mrefu kwa mazingira na jamii ya eneo hilo.
Chalamila ambaye alikuwa mgeni rasmi katika tukio hilo amesisitiza umuhimu wa kushirikiana kwa dhati kati ya serikali na wananchi katika kuimarisha mazingira na kukabiliana na changamoto za mabadiliko ya tabianchi.
Aliongeza kuwa wananchi wanapaswa kuchukua jukumu la kulinda miti hiyo mara baada ya kupandwa ili kuhakikisha ufanisi wake unadumu.
Amesema, “Tunahitaji usimamizi na ufuatiliaji wa karibu kutoka kwa viongozi wa maeneo haya, kwa kushirikiana na jamii, ili kuifanya miti hii kuwa sehemu muhimu ya maendeleo yetu ya kiuchumi na kimazingira.”
Alionyesha masikitiko yake juu ya uharibifu wa Mto Mpiji unaofanywa na baadhi ya watu, na ameweka wazi kuwa serikali haitasita kuchukua hatua kali dhidi ya wale wanaovunja sheria na kuharibu mazingira.
Amesema, “Ni muhimu kuhakikisha miti hii inasimamiwa vyema ili kutimiza lengo la kulinda mazingira na utunza kingo za mto huu na kuleta maendeleo endelevu kwa wananchi wa eneo hili.”
Mkurugenzi wa Bodi ya Maji Bonde la Wami/Ruvu Mhandisi Elibariki Mmassy amesema kuwa miti hiyo ya michikichi ina umuhimu mkubwa katika kuhifadhi wa mazingira na maji, kwani inasaidia kudhibiti mmomonyoko wa Ardhi.
Amesema michikichi pia ina faida za kiuchumi kwa kuwa inaweza kutoa mafuta na bidhaa nyingine za kibiashara, hivyo kuwawezesha wananchi kujiongezea kipato na kuchangia katika uchumi wa eneo hilo.
Uzinduzi huo pia unakuja wakati ambapo maeneo mengi nchini yanakabiliwa na athari za mabadiliko ya tabianchi, zikiwemo ukame na mmomonyoko wa ardhi.
Wataalamu wa mazingira wanasisitiza kuwa kupanda miti kunasaidia kuhifadhi unyevunyevu wa ardhi na kuongeza viwango vya mvua, jambo linalochangia kuboresha hali ya hewa.
Uzinduzi wa mpango huo umeshirikisha wakandarasi, na vikundi vya jamii, vikundi vya wasafisha Mto Mpiji, Kata ya Mabwepande.
Aidha, uzinduzi wa mradi huu umetoa fursa ya ushirikiano kati ya taasisi za umma na mashirika binafsi, pamoja na vikundi vya kijamii vikiwamo vikundi vya wasafisha Mto Mpiji, Kata ya Mabwepande.
Pia, mradi huu ni sehemu ya mkakati wa taifa wa kuongeza maeneo ya kijani katika miji mikubwa kama Dar es Salaam, ambao una lengo la kufikia malengo ya kitaifa na kimataifa ya uhifadhi wa mazingira.
Kupitia miradi huo, serikali inaamini kwamba inaweza kuimarisha uwezo wa wananchi kukabiliana na changamoto za mazingira, hasa zile zinazoletwa na kuongezeka kwa miji na shughuli za kibinadamu zinazochangia mmomonyoko wa ardhi na uharibifu wa vyanzo vya maji.
Kwa upande wake, Bodi ya Maji ya Bonde la Wami/Ruvu limesema wataendelea kutoa elimu kwa wananchi kuhusu faida za michikichi na umuhimu wa kuhifadhi vyanzo vya maji.
© 2024 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED