Raia wa Tanzania nchini Kenya wafanya maombi kuiombea nchi yao

By Neema Emmanuel , Nipashe
Published at 01:12 PM Aug 12 2024
Mchungaji Ezekiel Odera akongoza maombi kwa waumini wa kanisa lake.
Picha: Mpigapicha Wetu
Mchungaji Ezekiel Odera akongoza maombi kwa waumini wa kanisa lake.

RAIA wa Tanzania ambao ni waumini wa Taasisi ya dini ya ‘New Life Prayer Centre and Church’ ya jijini Mombasa nchini Kenya, wamefanya maandamano ya hisani katika kanisa hilo kuiombea nchi yao amani, kufuatia uchaguzi wa serikali za mitaa na uchaguzi mkuu unaotarajia kufanyika mwishoni mwa mwaka huu na mwaka kesho.

Wamefanya  maandamano hayo katika viunga vya makao makuu ya kanisa hilo (Mombasa), wakirejea historia kwamba zipo baadhi ya nchi ambazo zimekua zikiingia vitani mara baada  ya uchaguzi.

Kingozi wa kanisa hilo, Mchungaji Ezekiel Odera, alisema amani ni nguzo muhimu kwa anayepigiwa kura, anayepiga kura na wale watakaoongozwa.

Alisema Tanzania inajulikana kwamba ni nguzo ya amani katika bara la Afrika, sababu ambayo imekuwa ikiwavutia wengi kuipenda nchi hiyo, akiwemo yeye mwenyewe ambaye mara kwa mar amekuwa akiendesha mikutano yake ya huduma za kiroho.

"Kwa mwaka jana nimefanya mikutano minne nchini Tanzania na miwili hapa kwetu Kenya. Na watu wengi wamekuwa wakiniuliza kwanini naipenda sana Tanzania na mimi nasema mahali alipo Mungu amani ipo na mwanadamu akijua alipo Mungu ni lazima atamfuata.

1

"Nafurahi pia kuwaona watanzania wanakuja kwetu tufanye maombi ya kuomba amani, wametupenda, tumewapenda ,"alisema.

Mratibu wa kanisa hilo kwa upande wa Tanzania, Nabii Utukufukwabwana Peter, alisema kwa kawaida silaha hutengenezwa wakati wa amani na kutumika wakati vita, hivyo ni muhimu kufanya maombo kipindi hiki ili Tanzania iendelee kuwa na amani wakati na baada ya uchaguzi.

Alisema amani ni moja ya tunu la taifa la Tanzania, ambayo Rais  anafanya juhudi kubwa kuilinda na kuidumisha, hivyo waumini hao wanamuunga mkono kupitia huduma za kiroho.
2

"Watanzania kutoka takribani mikoa yote tumesafiri kuja huku ili kufanya maombi haya pamoja na kiongozi mkuu wa kanisa letu, ambaye amekuwa karibu na taifa letu wakati wote, iwe shida au raha raha.

"Tutakumbuka  wote kwamba nchi yetu ilipopata majanga ya kuporomoka kwa tope wilayani Hanang, mkoani Manyara, kiongozi wetu mkuu wa kanisa alikuwa Tanzania, akaguswa na ajali hiyo na kuchukua jukumu la kuchangia zaidi ya Shilingi millioni 100," alisema Nabii.
 
Kwa niaba ya watanzania wenzake, Rose Godfrey kutoka Bomang'ombe mkoani Kilimanjaro, alisema waumini wanaamini kila kitu kinawezekana kupitia maombi ya kanisa hilo, kama ambavyo yalimponya yeye saratani ya kizazi.