Prof. Mkenda ataka vyuo vya ufundi kuandaa mitaala itakayokidhi mahitaji ya soko la ajira

By Frank Monyo , Nipashe
Published at 03:48 PM Nov 09 2024
Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Profesa Adolf Mkenda.
Picha: Iman Nathaniel
Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Profesa Adolf Mkenda.

Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Profesa Adolf Mkenda, ametoa wito kwa Mamlaka ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi Stadi (VETA) kufanya mabadiliko kwenye mitaala ili kozi zinazotolewa ziendane na mahitaji ya soko la ajira na kuimarisha ustawi wa vijana wa Kitanzania.

Aidha amebainisha changamoto za ajira barani Afrika na .kusisitiza umuhimu wa taasisi za mafunzo kama VETA kushirikiana na waajiri wakati wa kuandaa mitaala na kuhamisha ujuzi ili kuboresha umuhimu wa kozi zinazotolewa.

Prof. Mkenda amesema hayo jana Novemba 8,2024 jijini Dar es Salaam wakati  katika kongamano la kuhitimisha mradi wa maendeleo ya ujuzi na ajira kwa vijana ulioanza mwaka 2021, ambapo wadau wa kijamii walitoa waraka wa pamoja kwa serikali kuhusu maendeleo ya ujuzi

amesisitiza kuwa, kupitia mabadiliko haya, VETA inapaswa kutoa mafunzo bora na yenye kuendana na teknolojia za kisasa ili vijana waweze kuwa na ujuzi unaotakiwa kimataifa.

Mkenda pia amehimiza ushirikiano kati ya VETA na sekta binafsi ili kuandaa mitaala inayozingatia mahitaji halisi ya soko la ajira.

Prof Mkenda ameongeza kuwa  licha ya jitihada za serikali na sekta binafsi kwenye kutatua changamoto za ajira kwa vijana, bado swala hili limeendelea kuwa tatizo nchini.

Amesema jitihada bado zinahitajika kwenye kuwawezesha vijana wanasomea masomo ya ufundi stadi ili kuhakikisha wanakuwa imara na kuweza kupenya kwenye soko la ajira.

Kwa upande wake,  Mtendaji  Mkuu wa Chama cha Waajiri Nchini (ATE) Suzan Ndomba-Doran amesema chama hicho kina mpango wa kuanzisha mabaraza ya ujuzi ili kushirikiana na wadau wengine kukuza kiwango  cha ujuzi kwa vijana pamoja na uwezo wa vyuo vya ufundi na vyuo vikuu ili kuzalisha vijana wengi zaidi wenye ujuzi.

Amesema, asilimia 79 ya nguvu kazi nchini ina ujuzi wa chini au haina ujuzi wa kutosha katika kuendeleza maendeleo endelevu ya kijamii na kiuchumi kwani asiliia 34.7% ya watanzania ni vijana kati ya miaka 15-35. Lakini wengi wao wanakutana na changamoto za kukosa ujuzi ambazo upelekea kushindwa kujiajiri au kuajiriwa.

 “katika kukabiliana na hilo, ATE kwa kushirikiana na Shirikisho la Viwanda vya Denmark na cha Wafanyakazi Tanzania (TUCTA), Wakala wa Maendeleo ya Vyama vya Wafanyakazi Denmark (DTDA) na washirika (Tanzania Union of Industrial and Commercial workers -TUICO & Researchers Academicians and Allied Workers Union - RAAWU), tunatekeleza mradi huu wa TVET unaolenga kukuza ujuzi ili kutengeneza vijana wanaoweza kuajiriwa wenye ujuzi wa ufundi stadi na ajira zenye staha nchini.

Amesema mpaka sasa mradi huo ulioanza mwaka 2021 umefanikiwa kupata mafanikio kadhaa pamoja na mambo ya kujifunza kwa ajili ya kuboresha ambapo wamepitia na kurejea mitaala kulingana na mahitaji ya soko kwa Fitter mechanics, umeme wa Majumbani na Viwandani, Uzalishaji wa Chakula, Majokofu na viyoyozi.

“pia tumetoa mafunzo kwa jumla ya wanafunzi 1098 ambapo asilimia 43 ni wanawake na asilimia 57 ni wanaume kwa  aina mbili za uanagenzi kwa kushirikiana na washirika huku pia mafunzo mengine yakitolewa kwa wakufunzi katika eneo la kazi kwa muda wa  wiki mbili ili waweze kujifunza teknolojia mpya pamoja na kulinganisha wanachokifundisha chuoni na uhalisia wa soko” amesema Doran.

5

Naye, Katibu Mkuu wa Raawu, Joseph Sayo amesema pamoja na kwamba mradi umepata mafanikio ya kuongeza ujuzi kwa vijana katika sekta mbali mbali ikiwemo baadhi yao kupata ajira lakini kunahitajika kuendelea kuwekeza katika mafunzo  ya ufundi stadi ili kihakikisha vijana wetu wanauwezo wa kushindana katika soko la ajira.

"Ujuzi unaotolewa katika vyuo vyetu umekuwa hauendani na Teknolojia iliyopo viwandani kwa sasa kitu  kinachopeleka  vijana wengi kushindwa kuajiriwa katika viwanda vyetu kwa kuwa ujuzi walionao wameupata kupitia mashine ambazo zimepitwa na wakati na hivyo wakifika viwandani wanaenda kujifunza upya.

"Tunaiomba serikali kupitia Wizara Elimu isaidie katika kuhakikisha vyuo vya ufundi vinapata nyenzo sahihi za kufundishia na kujifunzia ili vijana waweze kuendana na kasi ya soko la ajira duniani.

Aidha ameishuruku serikali ya Denrmark kwa kufadhili mradi huo uliopata mafanikio makubwa hivyo wanatumaini lwa ushirikiano huo, vyul vyetu vitaimarika zaidi na kuhakikisha vijana  wanajifunza kwa nadharia na vitendo ili waweze kuhitimu wakiwa na na ujuzi unaohitajika katika kuajiriwa ama kujiajiri.

Katika kongamano hilo, waajiri ambao walichukua wanafunzi wengi zaidi kwa ajili ya mafunzo kwa vitendo na Taasisi tano walitunukiwa vyeti.