Mtaalamu bingwa wa nyonga na magoti atua Dar

By Mwandishi Wetu , Nipashe
Published at 03:46 PM Aug 26 2024
Mtaalamu bingwa wa nyonga na magoti atua Dar
Picha: Mpigapicha Wetu
Mtaalamu bingwa wa nyonga na magoti atua Dar

MTAALAMU bingwa wa ubadilishaji wa nyonga na magoti kutoka hospitali kubwa nchini India ya Yashoda, Dk. Ram Mohan Reddy amewasili jijini Dar es Salaam kwaajili ya kambi ya matibabu hayo kwa watanzania.

Daktari huyo kwa kushirikiana na wataalamu wa ndani atafanya upasuaji huo kwenye kambi ya siku tano itakayofanyika katika hospitali ya Muhimbili Mloganzila  kuanzia leo Jumatatu hadi tarehe 30.

Aliwasili jana usiku katika uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere ambapo alipokelewa na wafanyakazi wa Global Medicare ambao wameratibu kambi hiyo kwa kushirikiana na Muhimbili Mloganzila.

 Akizungumza kwenye mapokezi hayo, Meneja Mkuu wa Global Medicare, Daniel Lazaro,  alisema wamefurahi kuona amefika salama nchini Tanzania na kwamba ujio wake utakuwa wa manufaa makubwa kwa watanzania wenye matatizo ya nyonga na magoti.

“Tunajua ni mara yako ya kwanza kuja kufanyakazi na madaktari wa hapa Tanzania  kwenye upasuaji wa aina hii lakini tunatarajia watanzania wengi watanufaika na ujio wako kwenye kambi hii ya siku tano itakayoanza katika hospitali ya Muhimbili Mloganzila,” alisema

Naye Dk. Reddy aliishukuru serikali ya Tanzania na taasisi ya Global Medicare kwa kuratibu vyema safari yake ya kuja nchini Tanzania na aliahidi kutoa huduma bora kwa wagonjwa watakaojitokeza kwenye kambi hiyo.

“Natarajia tunashirikiana vizuri sana na wataalamu wenzangu wa hapa nchini kwenye kambi hii ya siku tano na kwa huduma hii natarajia tutaongeza chachu ya ushirikiano baina ya Tanzania na India na tutabadilishana uzoefu wa kufanya upasuaji wa aina hii kwa wataalamu na watu wa hapa nchini watakaokuja kusoma India,” alisema

Mkurugenzi Msaidizi wa Huduma za Upasuaji wa hospitali ya Mloganzila, Goodlove   Mfuko, alisema hivi karibuni kuwa maandalizi yote yamekamilika na kwamba kwenye kambi hiyo watashirikiana na mtaalamu huyo Dk. Ram Mohan Reddy.

“Mtaalamu huyu atashirikiana na madaktari bingwa ambao ni wataalamu wa mifupa na ajali hapa Mloganzila, hii itakuwa mara ya pili kutoa huduma  kama hii kwani mara ya kwanza tuliwafanyia upasuaji wa kubadilisha nyonga na magoti wagonjwa 170 kwa mafanikio makubwa,” alisema

“Kwa hiyo kwenye kambi hii ambayo ni ya pili  tutashirikiana na daktari huyu mbobezi kutoka India kupata uzoefu ili tuweze kubadilishana naye uzoefu ili tuboreshe zaidi huduma zetu,” alisema

“Kwa hiyo watu wenye matatizo ya nyonga na magoti wafike Mloganzila mapema ili wafanyiwe uchunguzi wa mapema kwaajili ya kupewa hiyo huduma ya kubadilisha nyonga na magoti,” alisisitiza Dk. Mfuko.

5