VIONGOZI wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) wameeleza madhila waliyopitia wakiwa mikononi mwa polisi, huku wakitangaza kuwashtaki mahakamani Msajili Msaidizi wa Vyama vya Siasa, Sisty Nyahoza na Kamishna wa Operesheni na Mfunzo wa Jeshi la Polisi, CP Awadh Haji.
Katika mkutano wao na waandishi wa habari kwenye ofisi za makao makuu ya chama hicho Kinondoni, Dar es Salaam jana, viongozi hao walidai walipigwa na polisi kwa marungu na vifa vya umeme, huku wakilazimishwa kupandishwa kwenye magari.
Vilevile, wamedai kuwa kabla ya kukamatwa mkoani Mbeya wiki iliyopita, ofisi yao ya jijini Mbeya ilizingirwa na askari wenye silaha walizoziita "nzito", wakatolewa lugha mbaya na kuvunjiwa miwani yao.
Viongozi hao ni Mwenyekiti, Freeman Mbowe, Makamu Mwenyekiti Bara, Tundu Lissu, Katibu Mkuu, John Mnyika na Mwenyekiti wa Baraza la Vijana (BAVICHA), John Pambalu.
Katibu Mkuu wa Chama hicho, John Mnyika alidai alipelekwa eneo lenye giza na kushushiwa kipigo kikali kisha kurushwa kwenye gari ambako alimkuta Mwenyekiti wa Kanda ya Nyasa, Joseph Mbilinyi 'Sugu' akiwa "amepewa kipigo kikali".
Mnyika pia alidai kuchukuliwa simu zao na askari waliopeleka vituo vya polisi katika mikoa ya Songwe, Njombe na Iringa huku wakipewa amri ya kulala kifudifudi kwenye bati la gari aina ya landcruizer.
MBOWE
Mwenyekiti wa CHADEMA, Mbowe, alisema chama chao si cha kigaidi, hivyo ameagiza wanasheria wa chama kukutana haraka kuandaa mashtaka dhidi ya Naibu Msajili wa Vyama vya Siasa, Nyahoza na Kamishna Awadh.
“Ninawakumbusha tu Makamu wetu Mwenyekiti (Lissu) ambaye ni wakili ataongoza jopo hili. Kwa muda mrefu hatujamwona Lissu mahakamani, sasa tutamwona na leseni yake ya uwakili imesharejeshwa," alisema.
Mbowe pia alisema kuwa tangu warejeshe mikutano ya hadhara chama kimeifanya pamoja na maandamano na hawajawahi kumdhuru yeyote kwa kuwa si chama cha kigaidi, bali cha Watanzania.
"Hatuwezi kuwa chama cha kuadhibu wenye chama chao, hawa tutawawajibisha kama nilivyozungumza. Joseph Mbilinyi anaendelea na matibabu, alitamani kuja, yupo Dar es Salaam.
"Ni mgonjwa, jana (juzi) alilazwa Muhimbili, leo (jana) usiku akatoka, akarudishwa tena, wamemwumiza sana Kamanda Sugu kwa maelekezo ya Awadh," alidai Mbowe.
Mwenyekiti huyo pia alidai Kamishna Awadh alishiriki kuvunja miwani ya Katibu Mkuu Mnyika, akieleza kuwa viongozi wa CHADEMA wanabeba maumivu hayo kwa ajili ya taifa.
"Tunafanywa kondoo wa kafara si kwamba hatuna nyumba au vitanda vya kulala, tunatekeleza wajibu na wanachama muutekeleze.
“Kama tuna intelijensia katika nchi inayoweza kulichafua taifa zima matope, inatueleza tunaongozwa na watu wa namna gani. Hii operesheni imegharimu Jeshi la Polisi na nina hakika siwezi kusema kiasi, lakini yote tuliyoona mpaka kulipiwa nauli, watu kulipwa posho ni mamilioni ya walipakodi wa nchi hii.
“Hivi kweli fedha zetu sisi taifa maskini zinapaswa kutumika kwa mambo ya kihuni? Barua ya Msajili wa Vyama vya Siasa ambayo ni chimbuko la uhuni wote huu, inasema kiongozi wetu Katibu Mwenezi BAVICHA, eti alizungumza maneno haya na ndio mwanzo wa sakata hili," Mbowe alilalama.
LISSU
Makamu Mwenyekiti Bara, Lissu alidai polisi walikwenda kivita katika ofisi zao za Kanda ya Nyasa, jijini Mbeya, wakiwa na silaha za moto, mabomu na fimbo za umeme.
Alisema kuwa Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mbeya, Benjamin Kuzaga, aliingia ndani walimokuwa na kuwaeleza alitaka kuzungumza na viongozi.
"Tulimkaribisha, aliingia yeye na Mkuu wa Upelelezi wa Makosa ya Jinai Mkoa wa Mbeya (RCO) na wasaidizi wao wawili.
"Tulizungumza na hoja ya Kamanda Kuzaga ilikuwa kwamba, wanahitaji kumchukua Twaha Mwaipaya, kiongozi aliyekuwa anaratibu shughuli za BAVICHA kutoka Makao Makuu Dar es Salaam na Makamu Mwenyekiti wake.
"Tulimwuliza 'unawachukua unawakamata au la? Alisema anawachukua kwa lengo la kuwakamata. Tukashauriana kwa pamoja kwamba, kwa vile ndio viongozi wetu, tulimwomba atupe muda ili watueleze maandalizi ndipo aondoke nao. Alikubali na kutupa dakika 40," alidai Lissu na kueleza kuwa baadaye viongozi hao wawili walichukuliwa na polisi.
Alisema baada ya hapo giza likiwa limeingia, wakiwa wamezingirwa na polisi, Kamanda Kuzaga aliwaeleza hakuna mtu kutoka wala kuingia.
Alisema wakati wakijiandaa kwa mkesha akiwa ameahidi "kutoa shule usiku kucha juu ya mambo ya nchi", polisi waliozingira ofisi hiyo waliingia ndani na kukamata watu wakiongozwa na Kamanda Kuzaga.
"Ndipo kipigo kikaanza kwa kutumia marungu, yakiwamo ya umeme. Na mimi nikavurumishwa na 'kamguu kangu', ikawa vurumai, kilichotokea kwangu angalau, Kamanda Kuzaga alikuja akanichukua akanitoa nje akanikabidhi kwa RCO akamwambia ‘mpeleke kwenye gari lako’ huku nyuma nikaacha kipigo kinaendelea," alidai.
Lissu alidai kuwa akiwa katika gari, Kamishna Haji alihoji alikokuwa na kufuatwa kwenye gari la RCO na kupelekwa alikokuwa na ndipo akachukua kofia yake na miwani na kumwamuru apande gari la wazi la polisi.
"Akaniambia ‘panda hilo gari’, nikamwambia 'siwezi, sina mguu', akaniambia ‘umekuja kutafuta nini hapa?’ Kwa kuwa nilishindwa kupanda, akawaamuru wale askari wanibebe na kuniingiza katika Land Cruiser, nikasukumizwa kwenye uvungu wa viti vyao.
"Nikalala pale na baadaye walinirudishia kofia yangu na kofia ya mtu mwingine na miwani," Lissu alisimulia.
MNYIKA
Katibu Mkuu Mnyika alisema alikataa kutoa maelezo yake na kueleza kuwa atatoa mahakamani, akidai ndiyo sababu ya kupewa kosa la kutotii amri ya polisi kulikosababisha kuingizwa mahabusu isiyo na kitanda na alikolala hadi asubuhi kisha akasafirishwa kwa gari alilolitaja "zuri kiasi" lakini hakupewa simu zake.
"Nilipofika Kituo Kikuu cha Dar es Saalm usiku wa manani, niliwauliza askari niliokabidhiwa kwao, nimetuhumiwa kwa kosa lenye dhamana, kwanini sijapewa dhamana, sijatibiwa, sijaonana na wakili wangu wala familia?
"Waliniambia 'usiwe na wasiwasi, tunawaruhusu watu wa Njombe', baadaye waliniambia nijidhamini mwenyewe na niripoti polisi Agosti 15, 2024," alidai.
Mnyika alidai kuwa aliwaomba wamwitie usafiri wa kukodi jijini Dar es Salaam, wakamjibu watampeleka kwa usafiri wa polisi, akapelekwa hadi nyumbani kwake ambako alifika saa tisa usiku.
"Polisi walitupiga bila sababu ya kutupiga, ni kama walitumwa kufanya udhalimu kwa kuwa walikuwa wanaelewa wanachokifanya, niliona ni kaburi la 4R za Rais Samia Suluhu Hassan," alidai Mnyika.
PAMBALU
Mwenyekiti wa BAVICHA, Pambalu, alisema aliingia nchini Agosti 12, mwaka huu, akitokea Marekani na aliwatafuta viongozi wa chama bila mafanikio hadi alipompata Mwenyekiti Mbowe, ili wakatoe msaada wa kibinadamu na kisheria, wakisafiri kwa ndege usiku.
"Tulifika saa 5:15 usiku, wakati tunashuka Mwenyekiti hakushuka, nilivyomfikia, akaniambia 'ninaona kuna askari wengi', akauliza 'kuna mheshimiwa yoyote tunasafiri naye?', tulivyoshuka walinikamata wakanipeleka mbali na mwenyekiti, kisha tukapakizwa kwenye magari ya polisi.
"Tulipelekwa ofisi ya Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mbeya. Tukiwa uwanja wa ndege, tulihoji kosa la kukamatwa, askari walijibu hawajui, bali wakubwa wao watatuambia kwanini tumekamatwa. Tulikaa kwa saa mbili, tukihojiwa, mwenyekiti hakusema chochote, mimi niliandika jina langu tu," alisema.
Nipashe ilimtafuta Msemaji wa Jeshi la Polisi Tanzania, Kamishna Msaidizi, David Misime, kwa ajili ya kupata ufafanuzi wa madai ya CHADEMA dhidi ya polisi, lakini simu yake haikupokewa.
© 2025 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED