VIONGOZI wa vyama vya upinzani wamezidi kulia na maumivu baada ya kudai kuwa zaidi ya asilimia 60 ya wagombea wa nafasi za uenyekiti na ujumbe wa Serikali za Mitaa, Vijiji na Vitongoji, wameenguliwa.
Kutokana na hali hiyo, wamewasisitizia wagombea walioenguliwa kuwasilisha mapingamizi kwa wasimamizi wasaidizi wa uchaguzi kwenye maeneo yao.
Pia wameitaka Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI), kuwaelekeza wasimamizi kufungua ofisi ili kuyapokea mapingamizi ya walioenguliwa.
Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam jana, Kiongozi ACT-Wazalendo, Dorothy Semu, alisema asilimia 60 ya wagombea wa chama hicho nchi nzima wameenguliwa.
Alisema wanachama wa chama hicho walijiandaa kikamilifu kushiriki uchaguzi lakini kilichofanyika ni hujuma dhidi yao.
Alisema wagombea wengi wameenguliwa kinyume cha kanuni na taratibu za uchaguzi, kwa madai kuwa katika baadhi ya maeneo, fomu za wagombea wao zilichezewa.
“Hatukutegemea yale yaliyotokea kwenye uchaguzi mwaka 2019 na 2020, yangejirudia hasa ukizingatia kwamba tumekuwa na muda mrefu wa kufanya maridhiano. Kibaya zaidi ni kwamba wagombea walioenguliwa ni wa vyama vya upinzani. Tumesikitika sana,” alisema.
Dorothy aliwaelekeza wagombea walioenguliwa, kuweka mapingamizi na kwamba chama hicho kinawasiliana na vyama vingine vya upinzani, ili kuona hatima ya wagombea walioenguliwa.
Kwa upande wake, Chama Cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), kimeitaka TAMISEMI ielekeze wasimamizi wasaidizi wa uchaguzi kuwapo ofisini ili kupokea mapingamizi yao, wafungue mlango mwingine wa kuyapokea ikiwa watendaji wataendelea kukaidi amri ya kuwa ofisini.
Mkurugenzi wa Itifaki, Mawasiliano na Mambo ya Nje, CHADEMA, John Mrema, alisema wanaitaka TAMISEMI kuchukua hatua za kinidhamu dhidi ya watendaji na wasimamizi wote, ambao wanaharibu uchaguzi kwa makusudi huku wakijua kufanya hivyo kunaweza kulitumbukiza taifa katika machafuko.
Mrema alisema CHADEMA kinataka kujua sababu za kuondolewa kwa wasimamizi wa uchaguzi katika nafasi zao na kuteuliwa wapya baada ya kufanya uteuzi juzi, kwani wanaamini kuwa TAMISEMI ndio iliyotoa maelekezo hayo.
Alisisitiza wagombea walioenguliwa kukata rufani na kuziwasilisha katika ofisi za watendaji, kama zimefungwa ofisi hizo wakae hapo mpaka ofisi zitakapofungulia.
Alisema juzi kuwa Waziri wa TAMISEMI, Mohamed Mchengerwa, alisema wagombea walioenguliwa wakate rufani na kuwa rufani hizo zitasikilizwa kwa haki, lakini wanashangaa kupokea taarifa kuwa ofisi za watendaji wa mitaa, vijiji na vitongoji zimefungwa kuanzia Bukoba Vijijini, Dar es Salaam, Simiyu, Solwa, Bariadi na maeneo mengine nchini.
Naibu Katibu Mkuu Bara wa Chama cha Wananchi (CUF), Magdalena Sakaya, alisema zaidi ya asilimia 70 hadi 80, ya wagombea wake wameenguliwa kinyume cha utaratibu.
Alisema baadhi ya wagombea wameenguliwa kwa kutobandika picha na wengine wameambiwa wamekosa sifa ya kuteuliwa, bila kupewa maelezo ya kanuni iliyowakosesha sifa.
“Wapo walioenguliwa kwa kutobandika picha, wakati hilo siyo hitaji la kikanuni kwa uchaguzi wa mwaka huu. Wakati wagombea wa CUF na na vyama vingine vya upinzani wakienguliwa kwa sababu zisizo na mashiko.
“Wako wagombea wa CCM, ambao walistahili kabisa kuenguliwa kikanuni, lakini wamepitishwa,” alidai huku akitoa mfano kwamba, wagombea wa chama tawala katika Kata ya Pahi, wilayani Kondoa, Mkoa wa Dodoma, wamedhaminiwa na chama ngazi ya kata, badala ya ngazi ya chini ya chama hicho, jambo ambalo ni kinyume cha kanuni za uchaguzi na wamepitishwa.
Alisema badala yake, katika kata hiyo, wagombea wote wa CUF wameenguliwa kwa sababu zisizo za kikanuni.
“Hali imekuwa mbaya zaidi maeneo mengi ya wilaya ya Kinondoni. Takribani kata zote za Mtwara Mjini, Kondoa Vijijini, Tunduru, Manispaa ya Morogoro, Kilombero, Ifakara na Morogoro Vijijini kwa ujumla, zaidi ya asilimia 80 ya wagombea wetu wameenguliwa,” alisema na kubainisha kuwa hali hiyo imetokea pia katika vijiji na vitongoji katika wilaya za Liwale na Kilwa.
Kiongozi huyo alimwomba Rais Samia Suluhu Hassan, kunusuru uchaguzi huo, kwa kuielekeza TAMISEMI, iwarudishe wagombea wote wa upinzani walioenguliwa kwa kile alichokiita kwa hila.
“TAMISEMI ihakikishe wagombea wote wa CCM walioteuliwa kimakosa licha kukiuka kanuni kule Pahi na maeneo mengine wanaenguliwa,” alisema.
Alisema uchaguzi huo ambao umepangwa kufanyika Novemba 27 mwaka huu, wanauchukulia kama kipimo cha maridhiano yaliyoasisiwa na Rais Samia, alipoingia madarakani mwaka 2021.
POLISI WAONYA
Wakati huo huo, Jeshi la Polisi limeonya kuwa yeyote anayepanga na kuhamasisha uhalifu kupitia vyama vya siasa, kuacha mara moja kwani linafuatilia kwa karibu.
Taarifa iliyotolewa juzi na Msemaji wa Jeshi la Polisi nchini, Naibu Kamishna (DCP) David Misime, ilisema kuna chama cha siasa kimepanga na kinahamasisha wafuasi kwa njia mbalimbali ikiwapo kukutana, kupigiana simu, kutumiana ujumbe na kwa kutumia makundi sogozi, kudhuru watu na kuharibu ofisi za serikali.
“Hatuko tayari kumvumilia mtu, kikundi cha watu au chama chochote cha siasa kinachopanga uhalifu wowote ili kutaka kuvuruga amani ya nchi. Tutamchukulia hatua kali kwa mujibu wa sheria za nchi,” alisema.
Alisema jeshi hilo limejipanga kuhakikisha kuwa wananchi wanafanya shughuli zao za kujiletea maendeleo na kushiriki uchaguzi huo katika mazingira yenye amani, utulivu na usalama, hivyo wasiwe na hofu.
IMEANDALIWA na Restuta James na Jenifer Gilla.
© 2024 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED