WAZIRI MKUU, Kassim Majaliwa, amefanya mazungumzo na Balozi wa Umoja wa Ulaya (EU) nchini, Christine Grau, Ofisini Ndogo ya Waziri Mkuu Magogoni, jijini Dar es Salaam.
Katika mazungumzo hayo leo, Februari 18, 2025, Majaliwa amesema Tanzania itaendelea kukuza na kuimarisha ushirikiano wa kibiashara na uwekezaji na nchi EU.
“Inatia faraja sana kuona kuna ukuaji wa biashara na uwekezaji kati ya Tanzania na nchi za Umoja wa Ulaya, Umoja wa Ulaya umewekeza takriban euro bilioni tatu nchini, hii kwa kiasi kikubwa imechangia kutengeneza ajira na makusanyo ya kodi.”
Amesema kuwa Tanzania itaendelea kuweka mazingira wezeshi ya uwekezaji, ili kuzivutia sekta binafsi kushiriki katika shughuli za maendeleo.
Kadhalika, Majaliwa amesema kuwa Tanzania inathamini msaada mkubwa ambao unatolewa na EU, katika kuchangia shughuli za maendeleo nchini.
“Katika kipindi cha 2021-2027, Umoja wa Ulaya umetenga euro milioni 703, ili kusaidia mipango mbalimbali ya maendeleo nchini Tanzania, tunakushukuru hasa kwa kujitolea kwenu kuimarisha ushirikiano huu.”
Awali, Majaliwa alikutana na Balozi wa Jamhuri ya Korea, Ahn-Eun-Ju ambaye alimweleza kuwa Tanzania inajivunia ushirikiano na nchi hiyo, kwenye sekta mbalimbali za maendeleo.
“Tunatambua kuwa makampuni ya Jamhuri ya Korea yamewekeza katika sekta mbalimbali nchini Tanzania, kama vile viwanda, usafirishaji na ujenzi, hivyo kuchangia maendeleo ya nchi zetu. Tunathamini uwekezaji huu. ”
Majaliwa alimweleza balozi huyo kuwa, aone namna ya kuwawezesha vijana wa Kitanzania kupata nafasi za kazi nchini Korea, hasa kwenye sekta ya uzalishaji.
“Kwa upande wetu sisi tutahakikisha Watanzania wanakuwa na vigezo stahiki vinavyohitajika ili waweze kufanya kazi. ”
Balozi Ju alimweleza Majaliwa kuwa katika kipindi chote atakachohudumu kama balozi nchini, atahakikisha anasimamia na kuendeleza masuala ya uwekezaji kwa faida ya nchi zote mbili.
© 2025 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED