Macha apongeza serikali, TANAPA ujenzi barabara

By Mwandishi Wetu , Nipashe
Published at 02:53 PM Sep 05 2024
Macha apongeza serikali,  Tanapa ujenzi barabraba
Picha: Mpigapicha Wetu
Macha apongeza serikali, Tanapa ujenzi barabraba

MKURUGENZI wa Kampuni ya Utalii ya Wolway Trekking Tanzania Limited, John Macha amepongeza hatua zinazochukuliwa na Serikali kupitia TANAPA kuboresha barabara zilizoathiriwa na mvua pamoja na wingi wa magari ya utalii yanayopita kwa siku.

Katika barabara hiyo inakadiriwa takribani magari 300 mpaka 500 yaliyobeba watalii hupita.

Mkurugenzi huyo ameyasema hayo leo alipozungumza na waandishi wa habari waliotembelea eneo hilo.

Macha aliyasema hayo mbele ya Kamishna ya Uhifadhi wa Shirika la Hifadhi za Taifa (TANAPA), Nassoro Juma Kuji, ambaye alifanya ziara ya kukagua matengenezo yanayoendelea kufanyika katika barabara ya Naabi hadi Seronera.

Kutokana na hali hiyo wadau hao wamependekeza kujengwa kwa barabara yenye tabaka gumu katika hifadhi hiyo ikiwa ni mwarobaini wa tatizo la barabara.

“Niipongeze Serikali kwa matengenezo haya ya barabara kutoka Seronera mpaka Golini tunafahamu hii ni kazi kubwa mnaifanya na tunaomba muendelee nayo lakini kwa ufumbuzi wa kudumu kuwe na jawabu la kudumu kwa sababu magari ni mengi mtakuwa mnafanya zoezi hili ndani ya wiki mbili mpaka tatu mnarudia zoezi hili.

“Kwa hiyo lile wazo Serikali kupitia Serengeti la kuwa na tabaka gumu la kudumu lingekuwa wazo zuri sana wakati huu tungesahau matengenezo haya ya mara kwa mara na hata kuongeza gharama ni bora tuingie gharama kutengeneza barabara itakayokaa muda mrefu hata kama ni gharama kubwa,” amesema Macha

Januari 26, 2024 Kamishna wa Uhifadhi wa Shirika la Hifadhi za Taifa Tanzania (TANAPA), Nassoro Juma Kuji alifanya ziara ya kukagua miundombinu katika Hifadhi ya Taifa Serengeti na kuiagiza menejimenti ya hifadhi hiyo, kushughulikia kwa haraka maeneo korofi ya barabara ndani ya hifadhi ili watalii wafikie azma yao ya kutembelea Hifadhi ya Taifa Serengeti.

Kutokana na hali hiyo aliilekeza Menejimenti ya Hifadhi ya Taifa Serengeti kurekebisha maeneo yote korofi na kuhakikisha kuwa hakuna maeneo ambayo hayatapitika licha ya uwepo wa mvua kubwa zilizonyesha pamoja na ongezeko kubwa la magari ya utalii ili kupunguza adha kwa wageni.

“Licha ya changamoto ya mvua kubwa zinazoendelea hatuwezi kusubiri ziishe tumeazimia kushughulikia kwa haraka maeneo yote korofi ikiwa ni hatua za haraka, lakini lengo kuu ni kuhakikisha barabara hizi zinakuwa na tabaka gumu, haya ni maagizo yangu kwa menejimenti kuhakikisha barabara zote zinapitika wakati wote,” amesema Kamishna Kuji.

Aidha, aliishukuru serikali kwa kutoa fedha kwa ajili ya kukarabati miundombinu ambayo kwa kiasi kikubwa imeathiriwa na mvua kubwa zinazoendelea kunyesha nchi nzima.

Pamoja na hali hiyo, Kamishna Kuji amebainisha kuwa TANAPA inafanya kila liwezekanalo kuhakikisha miundombinu yote katika Hifadhi za Taifa nchini inaboreshwa ili kukidhi matamanio ya wageni wanaotembelea hifadhi hizo zilizosheheni sifa lukuki za kuwa na utajiri mwingi wa bayoanuai.

Naye, Kamishna Msaidizi wa Uhifadhi anayeshughulikia miundombinu Mhandisi Dk. Richard Matolo alibainisha kuwa Shirika limekuwa likitumia teknolojia mbalimbali kutafuta mwarobaini wa changamoto za barabara na kubainisha kuwa mwaka huu hali imekuwa tofauti kutokana na mvua kubwa zilizonyesha  tofauti na miaka mingine.

“Shirika limefanya majaribio mbalimbali na kuja na teknolojia ambazo zitapelekea barabara hizi hususani hii ya Naabi iwe inapitika wakati wote tafiti nyingi zilionekana haziwezi kuleta matokeo chanya katika maeneo haya kutokana na asili ya udongo wa hifadhi zetu hivyo kutokana na stadi zote imethibitika kuwa tunaweza  kutumia tabaka gumu kujenga barabara hizi,” amesema  

Mkuu wa Hifadhi ya Taifa Serengeti, Kamishna Msaidizi wa Uhifadhi Stephen Msumi alisema kuwa menejimenti ya Serengeti imejipanga kuhakikisha maeneo korofi yanarekebishwa na kutoa rai kwa waongoza watalii kuzingatia sheria na taratibu mbalimbali katika hifadhi ikiwemo kudhibiti mwendokasi alama mbalimbali za barababra ili kuepusha madhara yanayoweza kujitokeza.

Hifadhi ya Taifa Serengeti hivi karibuni imekumbwa na changamoto ya barabara kutokana na mvua kubwa zilizonyesha Nchini na kuharibu miundombinu ya barabara hizo Ukarabati unaofanywa na TANAPA utaondoa adha hiyo na kuzifanya barabara zote ndani Hifadhi ya Taifa Serengeti kupitika mwaka mzima.