MKUU wa Wilaya ya Shinyanga, Julius Mtatiro, amejibu kauli iliyotolewa hivi karibuni na Askofu wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania, Dayosisi ya Karagwe, Dk. Benson Bagonza kuhusu viongozi wanaosema kila kitu kimefanywa na Rais Samia Suluhu Hassan, hivyo wao kukosa haki ya kuendelea kuaminiwa.
Akijibu hoja hiyo, Mtatiro alisema sababu ya viongozi kufanya hivyo kila wanaposimama kwenye majukwaa ni kutokana na Rais Samia ndiye kiongozi wa nchi na majukumu yake yanatambulika kikatiba, kama mpitishaji wa kila bajeti inayopelekwa bungeni na kuzifanyia kazi.
Alitoa kauli hiyo juzi kwenye mkutano wa hadhara, uliofanyika katika viwanja vya Shule ya Msingi Town Manispaa ya Shinyanga na kuhudhuriwa na viongozi mbalimbali wakiwamo madiwani na mbunge wa Shinyanga, Patrobas Katambi.
“Kuna watu, tena na juzi nimemsikia kiongozi mmoja tena ana heshimika, anasema watu wanajikomba sana kwa Rais na Mwenyekiti wa CCM, eti kwa sababu kila kiongozi akisimama jukwaani anasema hili limefanywa na Rais, hebu niwakumbushe hii nchi inaongozwa na nani, bajeti zote ambazo zinapelekwa bungeni kupitishwa zinafanyiwa kazi na kuandaliwa na nani, kwa mujibu wa katiba yetu Rais ndiyo kila kitu,” alisema Mtatiro.
Aidha, alisema kila kitu kinachofanywa, amani pamoja na kodi ambazo hulipwa na wananchi, Rais ndiye anapanga na kwamba haiwezekani kusema mafanikio yaliyopo hapa nchi yanaletwa na kila mtu tu, na ukimtaja Rais wa Tanzania unawataja Watanzania wote.
Mbunge wa Shinyanga Mjini, Patrobas Katambi, alisema huduma mbalimbali zimeendelea kuboreshwa jimboni humo ikiwa ni pamoja na ujenzi na ukarabati wa madaraja, ambayo yalikuwa kero kwa wananchi, huduma za afya, elimu ambako zimejengwa shule mpya tatu za sekondari.
© 2025 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED