Changamoto za miundombinu ya barabara Mkuranga kero kwa wananchi

By Yasmine Protace , Nipashe
Published at 06:42 PM Nov 09 2024
Mkuu wa Wilaya ya Mkuranga, Hadija Nasir
Picha: Mtandao
Mkuu wa Wilaya ya Mkuranga, Hadija Nasir

Wilaya ya Mkuranga mkoani Pwani inakabiliwa na changamoto kubwa ya ubovu wa miundombinu ya barabara, jambo linalozuia maendeleo na kusababisha kero kwa wananchi.

 Hayo yalisemwa na Mkuu wa Wilaya ya Mkuranga, Hadija Nasir, wakati wa kikao cha kawaida cha Baraza la Madiwani kilichofanyika wilayani hapo.

“Wilaya ya Mkuranga inakabiliwa na kilio kikubwa cha barabara kutoka kwa wananchi,” alisema Hadija, akibainisha kuwa maeneo mengi wilayani humo yanahitaji zaidi ujenzi wa madaraja kuliko barabara za kawaida kutokana na jiografia ya eneo hilo. Alisisitiza kuwa bajeti ya shilingi bilioni 3.5 haitoshi kukidhi mahitaji ya ujenzi na matengenezo ya barabara katika wilaya yenye mtandao wa barabara unaofikia kilomita 800.

Pamoja na changamoto hiyo, Mkuu wa Wilaya alisema wameomba nyongeza ya fedha ili kuboresha miundombinu hiyo na kwamba fedha za ziada zitakapotolewa, zitasaidia kuhakikisha barabara zinajengwa kwa viwango bora na madiwani hawataachwa bila msaada. Hata hivyo, alibainisha kuwa wameshaanza kuwapokea wakandarasi tangu Oktoba 13, lakini wamekwama kuwaweka kwenye maeneo ya kazi kutokana na ukosefu wa fedha za awali, hali inayoweza kusababisha wakandarasi hao kutoroka na mitambo yao.

Diwani wa Kata ya Mkamba, Hassan Dunda, alisema wilaya hiyo imeendelea vizuri katika sekta nyingi, lakini upande wa barabara umesalia nyuma, na hali hiyo imekuwa changamoto kwa wananchi kutokana na ubovu wa barabara. Aliongeza kuwa wakandarasi waliopita walifanya kazi nzuri, lakini baadhi ya wakandarasi wa sasa wanashindwa kutekeleza majukumu yao kwa ufanisi, jambo linalochangia kuharibika kwa miundombinu ya barabara.

Kwa upande wake, Meneja wa TARURA Wilaya ya Mkuranga, Mhandisi Silas Dilliwa, alisema kuwa kwa mwaka wa fedha 2024/2025, zaidi ya shilingi bilioni moja imeidhinishwa kwa ajili ya matengenezo ya barabara wilayani humo. Pia alifafanua kuwa kiasi cha zaidi ya shilingi bilioni mbili kimepangwa kwa bajeti ya maendeleo kwa ajili ya matengenezo zaidi ya barabara katika wilaya hiyo.

Hadi kufikia Septemba 30 mwaka huu, Wilaya ya Mkuranga ilikuwa imeshapokea zaidi ya shilingi bilioni 18 kwa ajili ya usimamizi na utawala wa miradi ya maendeleo, ingawa fedha za maendeleo za mwaka huu bado hazijapokelewa, hali inayoleta changamoto kwenye utekelezaji wa miradi iliyopangwa.