ASKOFU Mkuu mstaafu wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT), Dk. Frederick Shoo, amewataka Watanzania kujitokeza kushiriki ipasavyo katika Uchaguzi wa Serikali za Mitaa na kuwachagua viongozi wanyenyekevu watakaowaletea maendeleo kwenye maeneo yao.
Vilevile, amewataka wananchi kutowabagua wagombea wanawake kwenye uchaguzi kwa kuwa uongozi wa Rais Samia Suluhu Hassan umedhihirisha wanawake wana uwezo wa kuongoza nchi.
Dk. Shoo aliyasema hayo juzi wakati wa ibada maalumu ya kuaga watumishi mbalimbali wastaafu wa KKKT Dayosisi ya Kati iliyofanyika mjini hapa.
Alisema katika uchaguzi huo uliopangwa kufanyika Novemba 27, mwaka huu na Uchaguzi Mkuu wa mwakani, Watanzania wanapaswa kuchagua wanawake na wanaume lakini walio wanyenyekevu, ambao jamii inawaona wana hofu ya Mungu katika utumishi wao wa kuwaletea maendeleo.
"Ndugu zangu, ni dhambi kubwa kudharau mchango wa wanawake katika maendeleo ya jamii, kwa maendeleo ya kanisa. Hivi sasa kuna mfumo dume ambao umejengwa kwamba wanawake hawawezi.
"Na mfumo huu haupo tu kwa jamii na kwenye siasa, bali upo hata kanisani kuwa wanawake hawawezi. Leo ninasimama hapa kuzungumza kwa niaba ya wanawake hawa, tuone mchango wao na tuwe na wazo kwamba 'wanawake wanaweza'," alisema.
Alitaka jamii kuwaunga mkono wanawake katika uongozi ili wazidi kusimamia maendeleo ya kanisa, jamii na miradi inayoanzishwa na serikali.
Kuhusu watumishi walioagwa ambao wamelitumikia kanisa kwa muda mrefu, Askofu Dk. Shoo alipongeza Dayosisi ya Kati kwa kuliona suala hilo na kutoa rai kwa madhehebu mengine ya dini nchini kuiga mfano huo ili kuwajengea heshima wazee wanaostaafu na familia zao.
Mkuu wa Mkoa wa Singida, Halima Dendego, alisema ibada hiyo ni uthibitisho kwamba kanisa hilo linawathamini wazee hao ambao walitumia muda wao mrefu wa maisha kulitumikia kanisa ambalo hivi sasa linaonekana kupiga hatua kubwa ya maendeleo katika nyanja mbalimbali.
"Nina ombi langu hapa leo, tuna uchaguzi hivi karibuni, niwaombe sana ndugu wananchi, wale wote ambao wamejitathmini na wanaona wanazo sifa, basi wasisite kugombea na sisi ndugu zao tutawachagua.
"Kuhusu salamu za Rais, tumeona hapa zilitolewa na Dk. Syprian Hilinti asubuhi, tunayo imani kubwa sana na mama yetu mpendwa anayetuletea maendeleo," alisema Dendego.
© 2024 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED