Askari wa Uhifadhi daraja la tatu (CR III) Arafat Saidi Miyimba (27) kutoka Hifadhi ya Taifa Serengeti amefariki dunia baada ya kukanyagwa na tembo wakati akitekeleza majukumu ya doria.
Tukio hilo lilitokea Leo Jumamosi Novemba 9,2024 majira ya saa nne asubuhi katika Kijiji cha Mrito, Wilaya ya Tarime, mkoani Mara.
Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na Afisa Uhifadhi Mkuu Kitengo cha Mawasiliano wa TANAPA, Catherine Mbena, tukio hili lilitokea wakati kikundi cha askari saba kilipokuwa katika doria ya kufukuza tembo waliokuwa wameingia kwenye maeneo ya wananchi ili kuwarudisha hifadhini.
Hata hivyo, kelele za wananchi wengi waliokuwa wakipiga mayowe zilimfanya tembo mmoja kuwa na taharuki na kuanza kuwakimbiza askari.
Katika purukushani hizo, askari Arafat alianguka na kukanyagwa na tembo huyo katika maeneo mbalimbali ya mwili wake, na kusababisha kifo chake papo hapo.
Mwili wa marehemu Arafat umehifadhiwa katika Hospitali ya DDH, Mugumu Serengeti na unatarajiwa kusafirishwa kesho kwenda kwao mkoani Morogoro kwa taratibu za mazishi.
© 2024 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED