Wataka Afrika kutilia mkazo nishati jadidifu

By Grace Mwakalinga , Nipashe
Published at 10:22 AM Jan 31 2025
Ofisa Mwandamizi wa Mabadiliko ya Tabianchi na Nishati Jadidifu wa Taasisi hiyo,  Baraka Machumu
Picha:Grace Mwakalinga
Ofisa Mwandamizi wa Mabadiliko ya Tabianchi na Nishati Jadidifu wa Taasisi hiyo, Baraka Machumu

WANAHARAKATI wa Mabadiliko ya Tabianchi na Mazingira, wametoa ushauri kwa viongozi wakuu wa Afrika kuzingatia teknolojia ya nishati jadidifu na endelevu katika utekelezaji wa mpango wa kuwafikishia umeme waafrika milioni 300 ifikapo mwaka 2030.

Kauli ya wanaharakati hao imekuja siku chache baada ya kumalizikia Mkutano wa Wakuu wa Nchi  wa Afrika kuhusu nishati(misheni 300) ulifanyika Januari 27-28, 2025 jijini Dar es Salaam.

Wakizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam, wanaharakati hao  wametoa wito kwa Serikali  za nchi za Afrika kulingana na fedha zilizotengwa, kuhakikisha wanatoa kipaumbe kwenye nishati jadidifu kama vile uzalishaji wa umeme wa  maji,  jua , upepo na joto ardhi.

Mratibu wa Taasisi ya GreenFaith Tanzania, Baraka Lenga, amesema endapo Serikali itajikita  katika kuwekeza katika nishati hizo jadidifu, itapunguza kwa kiasi kikubwa uchafuzi wa mazingira na mabadiliko ya tabianchi.

"Umeme ni nyenzo kubwa sana kwenye maisha  ya binadamu, mapendekezo  yetu kwa  Serikali ni kuwekeze kwenye nishati safi ambayo ni nishati ya jua, nishati ya upepo, nishati jotoardhi na nishati ya maji," ameeleza Lenga.

Naye Ofisa Mwandamizi wa Mabadiliko ya Tabianchi na Nishati Jadidifu wa Taasisi hiyo,  Baraka Machumu, amefafanua kuwa  kutokana na takwimu zilizotolewa katika mkutano huo, matumizi ya nishati jadidifu yataleta uendelevu na kufikia watu wengi zaidi.

Ofisa Mwandamizi wa Mabadiliko ya Tabianchi na Nishati Jadidifu wa Taasisi hiyo, Baraka Machumu.

"Mipango ni mizuri lakini tunapokuwa na mipango mizuri tuone mahitaji ya watu ni kitu gani. Ili kuhakikisha tunaepuka athari za mazingira na mabadiliko ya tabianchi na kupunguza utegemezi na kuleta haki sawa kwa jamii wananchi tunahitaji nishati mbadala," anasema.

Mkurugenzi wa Green Conservers, Ziada Kassim amesema  mwanamke ni mtu anayetakiwa kuzingatiwa zaidi katika suala la nishati kwa sababu ndiyo waathirika wakubwa nishati chafu.

Kwa upande wake  Steven  Selestin ambaye ni mkulima kutoka Tekelelo, Morogoro amesema umeme unamhusu kila mtu kuanzia anayeishi mjini hadi kijiji, kama wakulima wana uhitaji mkubwa wa nishati hiyo, hivyo anaiomba Serikali  kuhakikisha wanatumia njia mbadala kuwafikishia.
Mratibu wa Taasisi ya GreenFaith, Baraka Lenga, akizungumza na Waandishi wa Habari (hawapo picha)

Katika mkutano huo wa Wakuu wa Nchi za Afrika, umefanikiwa kupata ahadi za ufadhili wa Dola za Marekani Bilioni 40 kutoka Benki ya Dunia na Benki ya Maendeleo ya Afrika kwa ajili ya kuwezesha usambazaji wa umeme barani Afrika. Aidha, jumla ya nchi za Afrika 12 zimeingia kwenye Mipango Mahsusi wa Kitaifa kuhusu Nishati.

Rais Dk. Samia Suluhu Hassan ambaye alikuwa mwenyeji wa mkutano huo. alisema  Mpango Mahsusi wa Kitaifa kuhusu Nishati(National Enerrgy Compact) uliozinduliwa unalenga kuiwezesha Tanzania kuunganisha umeme kwa kaya milioni 8.3 zaidi ifikapo mwaka 2030.

Mratibu wa Taasisi ya GreenFaith, Baraka Lenga, akizungumza na Waandishi wa Habari (hawapo picha).