KAIMU Mkurugenzi Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Ofisi ya Zanzibar, Balozi Silima Kombo Haji, amesema ujio wa wajumbe wa nchi mbalimbali kutaka kuwekeza nchini unathibitisha umaarufu wa Zanzibar ulimwenguni.
Akizungumza na Sheikh el Amin Omer el Amin kutoka Sudan aliyefika ofisini kwake Maisara mjini Zanzibar kujitambulisha, alitumia fursa hiyo kumkaribisha kutembelea maeneo mbalimbali ya Zanzibar kujionea fursa za uwekezaji katika kisiwa hicho.
Balozi Kombo alimweleza Sheikh El Amin kuwa kwa sasa vipaumbele vya uwekezaji ndani ya Zanzibar ni biashara ya utalii, viwanda na uchumi wa buluu na kumshauri kufika Mamlaka ya Kukuza Uwekezaji Zanzibar (ZIPA) ili kupata maelezo zaidi ya maeneo yaliyo tayari kuwekezwa.
Alisema uchumi wa buluu umekusanya masuala ya uvuvi wa bahari kuu, utalii wa bahari kupitia visiwa vidogo vidogo, mafuta na gesi, pamoja na usafirishaji wa baharini.
“Watanzania na Wasudani ni ndugu na wana uhusiano wa muda mrefu hivyo kuja kuwekeza katika Kisiwa cha Zanzibar kutaimarisha zaidi undugu wao,” alisema Balozi Silima.
Naye Sheikh El Amin alisema ni mara ya kwanza kufika Zanzibar lakini amevutiwa na wananchi wake kutokana na ukarimu na ustaarabu waliyonao hasa kwa wageni wanaoingia nchini.
Alisema kabla ya kufika Zanzibar, alisikia sifa mbalimbali zinazotajwa kuwepo na kuzithibitisha baada ya kutembelea ambapo kwa sasa anatamani kuwa sehemu ya Zanzibar.
Sheikh El Amin alisema Zanzibar ina vivutio vingi na maeneo mbalimbali ya uwekezaji na kusema kuwa yupo tayari kuwekeza katika maeneo ya utalii Ili kukamilisha dhamira yake ya kuwa sehemu ya Zanzibar.
Sheikh El Amin ni mmoja wa Wasudan wanaoishi nchini Uingereza aliyefika Zanzibar kwa ajili ya kutafuta maeneo ya uwekezaji kupitia sekta ya utalii visiwani hapa.
© 2025 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED