Sh.bilioni 1.7 kuongeza nguvu miradi wananchi

By Shaban Njia , Nipashe
Published at 07:51 PM Feb 10 2026
Mkurugenzi wa Halmashauri hiyo Hadija Kabojela.
Picha: Mpigapicha Wetu
Mkurugenzi wa Halmashauri hiyo Hadija Kabojela.

Miradi ya maendeleo iliyoanzishwa kwa nguvu za wananchi katika vijiji mbalimbali vya Halmashauri ya Ushetu mkoani Shinyanga inatarajiwa kukamilika baada ya halmashauri hiyo kutoa kiasi cha Sh. bilioni 1.7 kutoka mapato ya ndani ili kuikamilisha miradi hiyo.

Fedha hizo zimetolewa kwa lengo la kukamilisha miradi ya zahanati, elimu, ofisi za kata na ujenzi wa majosho ya mifugo kwa wafugaji katika baadhi ya kata zenye mifugo mingi, hatua hiyo inalenga kuimarisha utoaji wa huduma za kijamii na kiuchumi kwa wananchi wa maeneo ya vijijini.
 
Mkurugenzi wa Halmashauri hiyo Hadija Kabojela aliyabainisha haya leo katika kikao cha Baraza la Madiwani cha robo ya pili ya mwaka wa fedha 2025/2026. 

Kikao hicho Baraza lilipokea na kujadili taarifa mbalimbali za utekelezaji wa miradi ya maendeleo katika kila kata.
 
Amesema katika robo hiyo, halmashauri imetoa Sh.bilioni 1.7 kwa ajili ya kukamilisha miradi iliyojengwa kwa nguvu za wananchi hususan majengo ya zahanati vijijini na kata, miundombinu ya elimu, ofisi za kata na majosho ya mifugo kwa wafugaji ili kuwapatia tabasamu wananchi.
 
Kabojela amesema, fedha hizo zimetolewa baada ya kuonekana miradi mingi ilifikia hatua nzuri, lakini ilikwama kutokana na ukosefu wa fedha za ukamilishaji na wamedhamiria kuona jitahada za wananchi zinafikia malengo. 
 
Mwenyekiti wa Halmashauri hiyo, Gagi Lala amesema bado kuna baadhi ya kata ambako miradi inaendelea kutekelezwa, hivyo kuagiza wahusika kuhakikisha miradi hiyo inakamilika kwa wakati na kuanza kutoa huduma kwa wananchi.
 
Ameonya dhidi ya uzembe na matumizi mabaya ya fedha, akisema hatua kali zitachukuliwa kwa yeyote atakayebainika kukwamisha miradi hiyo.
 
Diwani wa Kata ya Ulowa, Gabriela Kimaro amesema katika kata yake kuna ujenzi wa kituo cha afya umefikia hatua ya mwisho ya ukamilishaji na hivi karibuni walipokea fedha ili kukamilisha,hivyo ameahidi kuzisimamia ili zitumike kulingana na matumizi yaliyopangwa.