Mapya yaibuka kesi ACT Wazalendo dhidi ya ZEC

By Rahma Suleiman , Nipashe
Published at 04:56 PM Feb 10 2026
news
Picha Mtandao
Mapya yaibuka kesi ACT Wazalendo dhidi ya ZEC

DOSARI ya kisheria inayomhusisha wakili aliyesaini viapo vinavyohusu kesi iliyofunguliwa na Chama cha ACT Wazalendo kupinga hatua ya Tume ya Uchaguzi Zanzibar (ZEC) ya kuteketeza nyaraka maalumu za uchaguzi imesababisha iahirishwe.

Imeelezwa kuwa viapo hivyo vilivyowasilishwa mahakamani, wakili Usi Khamis Haji, ambaye  hakuwa na leseni halali ya uwakili kwa wakati husika.

Jaji wa Mahakama Kuu ya Zanzibar, Salma Ali Khamis, aliahirisha kutoa uamuzi wa kesi hiyo leo Febuari 10 Mahakama kuu Tunguu, hadi itakapotajwa Tena Februari 13 mwaka huu. 

Katika kikao cha kesi hiyo, Mahakama ilielezwa kuwa viapo vilivyowasilishwa na upande wa walalamikaji, vilisainiwa na wakili huyo bila kuwa na sifa za kisheria, jambo lililoibua hoja nzito ya kisheria iliyolazimu Mahakama kuahirisha kesi hiyo.

Jaji Salma Ali Khamis amesema Mahakama inahitaji muda zaidi kuchambua hoja hiyo kabla ya kutoa uamuzi wowote, ili kuhakikisha haki inatendeka kwa mujibu wa sheria na taratibu za Mahakama.

Kesi hiyo inahusu pingamizi la ACT Wazalendo dhidi ya uamuzi wa ZEC wa kuteketeza nyaraka zilizotumika katika uchaguzi, hatua ambayo chama hicho kinadai inaweza kuathiri haki na ushahidi unaoweza kuhitajika katika mashauri yanayohusiana na uchaguzi.

Upande wa ZEC ambapo iliwakilishwa na wakili wa serikali Said Salum Said uliieleza mahakama kuwa hatua ya kuteketeza nyaraka hizo iko ndani ya mamlaka ya kisheria ya tume hiyo, huku ukiomba kesi hiyo itupiliwe mbali, hoja ambazo zitasikilizwa na kutolewa uwamuzi baada ya kesi kuendelea Februari 13.

Kwenye kesi hiyo Mahakamani hapo kwa upande wa ACT ilisimamiwa na mawakili Rajab Abdallah Rajab na Suleiman Abdallah.

Aidha mawakili wa serikali walikuwa watetezi wa ZEC ni Said Salum Said, Muhamed Ame Muhamed,Mbarouk Suleiman Othman na Ali Issa Abdallah.