Bunge Burkina Faso lapigilia msumari marufuku vyama kisiasa

By Mwandishi Wetu , Nipashe
Published at 02:41 PM Feb 10 2026
Bunge la nchi hiyo
Picha: Mtandao
Bunge la nchi hiyo

Wabunge wa Burkina Faso, wameidhinisha kupigwa marufuku kwa vyama vya kisiasa, huku uongozi wa kijeshi ukijaribu kuimarisha mamlaka yake katika taifa hilo, uliochukuwa madaraka baada ya mapinduzi.

Wakati wa kikao cha bunge siku ya Jumatatu, wiki hii, wabunge 69 waliohudhuria kwa kauli moja walipiga kura kuunga mkono muswada uliowasilishwa na serikali. 

Muswada huo pia ulitupilia mbali sheria inayosimamia ufadhili wa vyama vya siasa na kampeni.

Kiongozi wa kijeshi wa Burkina Faso, Ibrahim Traore
Kulingana na Waziri wa Mambo ya Ndani wa nchi hiyo Émile Zerbo, hatua ya Januari 29 ilichochewa na hitaji la kupanga upya mazingira ya kisiasa ya kitaifa, kufuatia kile alichokiita mgawanyiko na mifarakano ya kijamii inayochochewa na kuzidisha kwa vyama vya kisiasa.

Ilifuatia kusimamishwa kwa mara ya kwanza kwa vyama vya kisiasa tangu 2022, wakati jeshi lilipochukua mamlaka katika mapinduzi.

Muda mfupi baada ya muswada huo kupitishwa bungeni, Zerbo amesema uamuzi huo utakaribishwa na watu wa Burkinabe, akisisitiza kuwa unaungwa mkono na mfumo wa kisheria.

Wachambuzi wanasema hii sasa inafungua njia kwa serikali ya kijeshi kufanya kazi bila upinzani - hatua iliyoshtumiwa na makundi kadhaa ya kutetea haki za binadamu.

Wiki iliyopita, Kamishna Mkuu wa Umoja wa Mataifa wa Haki za Kibinadamu, Volker Türk, alielezea marufuku hiyo kama hatua isiyo sahihi, na kuzitaka mamlaka kubadili uamuzi wao.

Türk alisema hatua hiyo inaondoa uwezo wa utendaji wa mashirika ya kutetea haki za binadamu.

"Badala ya kupiga marufuku vyama vya kisiasa na kuwafunga watu jela kwa kutoa maoni yao, mamlaka nchini Burkina Faso zinahitaji kutoa fursa kwa mashirika ya kiraia, ikiwa ni pamoja na watetezi wa haki za kibinadamu," alisema.

Wanajeshi katika nchi jirani za Mali na Niger walichukua hatua kama hizo mwaka jana, na kuibua wasiwasi kuhusu kurudi nyuma kwa demokrasia katika Afrika Magharibi.

Serikali za kijeshi za nchi tatu za AES zimeshutumiwa kwa kukandamiza mashirika ya kiraia, wapinzani wa kisiasa na waandishi wa habari.

CHANZO: BBC