LHRC yamvaa DC Magoti kuwaweka ndani watu 45

By Halfani Chusi , Nipashe
Published at 06:50 PM Feb 10 2026
LHRC yamvaa DC Magoti 
kuwaweka ndani watu 45
PICHA: MPIGAPICHA WETU
LHRC yamvaa DC Magoti kuwaweka ndani watu 45

KITUO cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC), kimelaani kitendo kilichofanywa na Mkuu wa Wilaya Kisarawe, Petro Magoti cha kuwakamata na kuwaweka ndani watu 45 waliodaiwa kwenda mahali huko kununua ardhi ambapo kwa maoni yake ununuzi huo ulikuwa batili.

Hayo yamesemwa leo februali 10,2026 Mkoani Dar es Salaam na Kaimu Mkurugenzi wa Kituo hicho, Fulgence Massawe alipozungumzia masuala mbalimbali ya haki za binadamu miezi miwili baada ya maadhimisho ya siku ya Kimataifa ya Haki za Binadamu.

Amesema hivi karibuni zilisambaa taarifa katika mitandao ya kijamii, zikimuonesha Magoti akitoa amri ya kuwekwa ndani jumla ya watu 45 waliodaiwa Kwenda Kisarawe kununua ardhi ambapo kwa maoni yake ununuzi huo ulikuwa batili kwa hoja kwamba kulikuwa na mazingira ya udanganyifu.

Katika kauli yake Magoti kabla ya kuwaweka ndani na kuwaachia baadaye amesema: “Ninaomba nitoe tena angalizo kwa watu wa Dar es Salaam  niliwambia usije Kisarawe kununua eneo bila kupita halmashauri, tumekamata gari linawatu kutoka Mbezi wamekuja kununua viwanja huku kwa Sh 200,000 sasa leo hapa wote 50 wanalala ndani kwa sababu hawajafuata utaratibu hawa wote wakitapeliwa shida inakuwa katika ofisi yangu” 

Massawe amesema kupitia hatua hiyo Msimamo wa LHRC wakuu wa wilaya hawana mamlaka ya kipolisi kwa mujibu wa sheria ya Mwenendo wa Mashauri ya Jinai na Sheria ya Jeshi la Polisi na polisi wasaidizi. 

“Inafahamika kwamba vipo vyombo vya kikatiba ikiwemo Jeshi la Polisi vilivyopewa mamlaka ya kushughulika na masuala ya jinai na si Mkuu wa wilaya, mkoa au Waziri kutokana na ukweli kwamba mkuu wa wilaya au mkoa hana vyombo vya kiupelelezi au kiuchunguzi.

“Tunatambua kwamba kwa namna moja ama nyingine wakuu wa wilaya na mikoa ni wenyeviti wa kamati za usalama katika maeneo yao ya kazi na wamepewa mamlaka chini ya sheria ya Tawala za mikoa ya kuweka watu mahabusu kwa muda wa masaa 24 au 48 lakini hata hivyo ni kwa mazingira maalum yasiyoangukia katika sheria ya Mwenendo wa Makosa ya Jinai na ile ya Jeshi la Polisi na polisi wasaidizi” amefafanua Massawe 

Amesema msimamo wao hakuna mahali popote ama ndani ya sheria za ardhi na nyinginezo katika mchakato wa uuzaji au ununuzi wa ardhi panapomhusisha mkuu wa Wilaya, Mkoa au Waziri badala yake Sheria ya Ardhi imeweka vyombo mahususi vyenye mamlaka hayo na inabainisha bayana taratibu ambazo zinapashwa kufuatwa na ama mnunuzi au muuzaji.

Amesisitiza wakuu wa Wilaya na Mikoa waache matumizi mabaya ya mamlaka hasa zinapohusishwa tuhuma za kijinai na kinyume chake Jeshi la Polisi litekeleze wajibu wake wa kikatiba. 

“Pia katika mchakato wa uuzaji au ununuzi wa ardhi vyombo vilivyopewa mamlaka chini ya Sheria ya Ardhi viachiwe jukumu hilo. Mfano mwingine ni ule wa aliyekuwa Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi Jery Slaa kuamriwa na mahakama kuu kanda ya Dar es Salaam kumlipa fidia mmoja ya mwananchi aliyevunjiwa jengo lake kutokana na amri ya Waziri” amesema  

Ameendelea kwamba hakuna mahali popote ndani ya Sheria ya Ardhi inayompa mamlaka Waziri kutoa amri ya ubomoaji au usitishwaji wa ujenzi isipokuwa mahakama pekee. 

Amesema kituo hicho kinaunga mkono mawaziri na viongozi wengine wa kisiasa kutatua kero za wananchi lakini inawaasa wajikite kwenye masuala ambayo wana mamlaka nayo na kwa yale ambayo yanaangukia mahakamani wawashauri wananchi kupeleka malalamiko yao huko.

KUHUSU UTEKAJI

Massawe amesema bado kuna ukamataji usiofuata utaratibu wa kisheria, matumizi yasiyo sahihi ya madaraka hususani kwa viongozi wa kisiasa na kuendelea kwa matukio ya watu kutekwa na kupotezwa.

Amekumbushia Julai, 2023 tume ya Kurekebisha mifumo ya haki jinai iliyoongozwa na Jaji Mkuu Mstaafu Othuman Chande ilipendekeza kuwa katika utekelezaji wa majukumu yake, Jeshi la Polisi linapaswa kufuata utaratibu wa kisheria ikiwa ni Pamoja na kujitambulisha na kumweleza mtuhumiwa juu ya tuhuma zinazomkabili na kituo anachopelekwa. 

“Mara kadhaa kumekuwepo na taarifa za ukamataji wa watu unaofanya na askari wasio na sare rasmi za Jeshi la Polisi hivyo kuzua taharuki miongoni mwa wananchi na kusambaa kwa taarifa kwamba muhusika ametekwa na watu wasiojulikana. 

“Taarifa hizi zinaposambaa kupitia vyanzo mbalimbali hasa mitandao ya kijamii ndipo Jeshi la Polisi hutoa taarifa kwamba mhusika anashikiliwa na Jeshi hilo kwa tuhuma mbalimbali” amesema Massawe

Itakumbukwa hivi karibuni aliyekuwa Waziri wa Mambo ya Ndani, George simbachawene alikemea kitendo cha baadhi ya polisi kufanya ukamataji kinyume cha sheria akiwataka kufuata sheria katika kutekeleza majukumu yao.   

Katika taarifa yake Massawe amekumbushia mkasa wa Godlove Materu mkazi wa Chapwa, Mji wa Tunduma, Wilaya ya Momba, Mkoa wa Songwe ambaye ni Mwenyekiti wa Chama cha Madereva wa Malori Tanzania aliyedaiwa kutekwa na watu wasiojulikana Februari 7 mwaka huu.

Amesema baada ya taarifa kusambaa katika mitandao ya kijamii zikidai kuwa ametekwa ndipo Jeshi la Polisi kupitia kwa Kamanda wa Polisi mkoa huo lilitoa taarifa kwa umma kuthibitisha kumshikilia mhusika.

“Tunapenda ifahamike kwa muujibu wa sheria kwamba ofisa wa Jeshi la Polisi anapokamata mtuhumiwa, anapaswa kujitambulisha jina lake, kituo anachofanyia kazi, kitambulisho chake, Kumweleza mtuhumiwa kwanini anamkamata, tuhuma zake na kituo anachompeleka.

Aidha anapaswa Kutoa fursa kwa ndugu kumtembelea kituoni hapo pamoja na haki yakupata uwakilishi kama ilivyoanishwa katika ibara ya 13(6)(a) ya Katiba Tanzania ya mwaka 1977 ikisomwa kwa pamoja na kifungu cha 55 cha Sheria ya Mwenendo wa Mashauri ya Jinai Sura ya 20.

Aidha kwa mujibu wa kifungu cha 51 cha Sheria ya Mwenendo wa Mashauri ya Jinai Sura ya 20 ikisomwa kwa pamoja na kifungu cha 226(7)(8)(9)(10) cha Kanuni za Kudumu za Utendaji wa kila siku kwa Jeshi la Polisi toleo la mwaka 2021 (The Police General Orders) ofisa wa Jeshi la Polisi atatakiwa ndani saa nne(4) tangu kukamatwa kwa mtuhumiwa awe amemfanyia mahojiano.

Amesema endapo muda huo utapita bila ofisa husika kufanya mahojiano tajwa, atatakiwa kufanya maombi kwa hakimu kuongeza muda usiozidi masaa nane (8) kwa mujibu wa kifungu cha 52 cha sheria hiyohiyo.

Amesema licha ya sheria hiyo, kumekuwepo na matukio watuhumiwa kuwekwa mahabusu zaidi ya muda unaoruhusiwa kisheria bila kufanyiwa mahojiano na hakuna maombi yeyote kwa hakimu.

WATU KUPOTEZWA

Massawe amesema taarifa za watu kudaiwa kutekwa au kupotezwa zimeendelea kuripotiwa na vyanzo mbalimbali hasa mitandao ya kijamii aklitolea mfano wa taarifa iliyotolewa kwa umma Februari 5 na shirika moja la kidini hapa nchini juu ya kutoonekana kwa padri Peter Rwezahura aliyekuwa akihudumu katika shule ya msingi Mkakatifu Bakhita iliyopo Musoma Mkoa wa Mara.

Amesema kwa mujibu wa taarifa hiyo padri huyo amepotea na hajaonekana kwa takribani miezi sita(6) sasa licha ya shirika hilo kufanya juhudi za kila aina kumsaka ikiwamo kutoa taarifa katika vyombo vya dola.

NINI KIFANYIKE?

Kituo hicho kimeshauri Jeshi la Polisi litoe taarifa kwa wakati pale linapomkamata mtu badala ya kusubiri uvumi wa kutekwa ili kuondoa taharuki katika jamii, Viongozi wa kisiasa wajiepushe na vitendo vya matumizi mabaya ya mamlaka yaliyo kinyume na utaratibu wa kisheria.

Aidha liwape haki ya dhamana wale wote wanaoshikiliwa kwa makosa ambayo yenye dhamana na kama kuna Ushahidi wa kutosha juu ya tuhuma zinazowakabili wafikishwe mahakamani kwa mujibu wa sheria.