Wadaiwa kumuua baba yao, kisa shamba ukoo

By Grace Mwakalinga , Nipashe
Published at 10:00 PM Feb 10 2026
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mbeya, SACP Benjamin Kuzaga.
Picha:Mtandao
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mbeya, SACP Benjamin Kuzaga.

Jeshi la Polisi Mkoa wa Mbeya, linawashikilia watu watatu wa familia moja kwa tuhuma za kumuua baba yao Jenti Segelela (87), mkazi wa Kitongoji cha Busoka–Masebe, Wilaya ya Kyela.

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mbeya, SACP Benjamin Kuzaga, amethibitisha tukio hilo Februari 10, 2026, na kuwataja watuhumiwa kuwa ni Solomon Mwambyale (68) pamoja na watoto wake wawili, Stephano Mwaisango (32) na Emmanuel Mwaisango (36).

Kwa mujibu wa Kamanda Kuzaga, mauaji hayo yalitokea Februari 7, 2026 katika Kitongoji cha Busoka, Kata ya Makwale, ambapo mzee huyo aliuawa kwa kukatwa na kitu chenye ncha kali.

“Watuhumiwa walikamatwa Februari 8, 2026 baada ya msako mkali, uchunguzi wa awali unaonesha kuwa chanzo cha tukio ni mgogoro wa ardhi ya ukoo unaochochewa na tamaa ya mali,” amesema Kuzaga.