Mkuu wa Mkoa wa Kilimanjaro, Nurdin Babu, amewataka wananchi wanaoishi pembezoni mwa Hifadhi ya Taifa ya Kilimanjaro (KINAPA), kuachana na tabia ya kujenga nyumba za mbao, badala yake kutumia matofali ili kujikinga na madhara ya majanga ya moto yanayojitokeza mara kwa mara katika maeneo hayo.
Babu amesema ujenzi wa nyumba za mbao umeendelea kuwa chanzo kikubwa cha madhara pindi moto unapotokea, ikiwemo wilaya za Siha na Rombo,hali inayosababisha hasara kubwa ya mali, ikiwamo kuhatarisha maisha ya wananchi.
Amesema ni wakati sasa kwa wananchi kubadilisha mifumo ya maisha, kuchukua tahadhari mapema na kujikinga na majanga ya moto kwa kujenga makazi salama na rafiki kwa mazingira.
Akizungumza leo Februari 10, 2026, wakati wa makabidhiano ya gari jipya la kisasa la Jeshi la Zimamoto na Uokoaji kwa Wilaya ya Siha, Babu amesema hatua hiyo ni sehemu ya jitihada za Serikali kukabiliana na uhaba wa magari ya zimamoto na kuimarisha uwezo wa kukabiliana na majanga ya moto na dharura nyinginezo.
Amesema ndani ya siku 100 za uongozi wake, Mkoa wa Kilimanjaro tayari umepokea jumla ya magari matatu ya zimamoto, hatua inayochochea ufanisi wa huduma za uokoaji.
Babu amesisitiza kuwa Wilaya ya Siha pamoja na wataalamu wa Jeshi la Zimamoto wanapaswa kulitunza gari hilo lenye thamani ya Sh.bilioni 1.2 ili lidumu na litumike ipasavyo katika kuokoa maisha na mali za wananchi.
Kaimu Mrakibu Kamanda wa Jeshi la Zimamoto na Uokoaji Mkoa wa Kilimanjaro, Gadafi Masoud, amesema gari hilo lina teknolojia ya kisasa, lina uwezo wa kuzima moto katika maeneo ya makazi, biashara, viwanda pamoja na maeneo yenye miundombinu finyu.
Akipokea gari hilo, Mkuu wa Wilaya ya Siha, Christopher Timbuka, amesema ni wajibu wao kulilinda na kulitunza gari hilo ili litekeleze malengo yaliyokusudiwa na Serikali, ikiwemo kutoa elimu ya msisitizo kwa wananchi kuhusu namna ya kuepuka majanga ya moto.
© 2026 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED