Anuani makazi zaidi ya mil 12 zaunganishwa mfumo makazi

By Sagini Hamis , Nipashe
Published at 01:40 PM Feb 10 2026
Waziri wa Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Angella Kairuki (kulia) akipokea maelezo kutoka kwa Afisa kutoka Mamlaka ya Mawasiliano nchini—TCRA (wa kwanza kushoto)
Picha: Mpigapicha Wetu
Waziri wa Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Angella Kairuki (kulia) akipokea maelezo kutoka kwa Afisa kutoka Mamlaka ya Mawasiliano nchini—TCRA (wa kwanza kushoto)

Serikali imesema jumla ya anuani za makazi milioni 12.9 na mifumo 29 ya taasisi za serikali na sekta binafsi imeunganishwa katika mfumo wa anuani za makazi (NaPa), ambazo hutumiwa katika utoaji wa huduma kwa wananchi.

Hayo yamebainishwa na Waziri wa Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Angella Kairuki, Februari 8, 2026 jijini Dar es Salaam na kusema hatua hiyo ni mwendelezo wa kuhakikisha nchi inakuwa taarifa sahihi za wakazi kuelekea Tanzania ya uchumi wa kidijitali.

Kairuki, amesema hayo katika Kilele cha Maadhimisho ya Wiki ya Anuani za Makazi yaliyoambatana na kauli mbiu “Anuani Mahiri na Ubunifu wa Huduma kwa Ukuaji Jumuishi” na kuongeza kuwa upatikanaji wa mifumo imara ya wakazi itasaidia kuimarisha utoaji na ufikishaji wa huduma kwa wananchi.

“Natambua kwamba baadhi ya taasisi zinatumia taarifa za makazi katika kutoa huduma kwa wananchi. Hadi sasa jumla ya anuani za makazi milioni 12.9 na mifumo 29 ya taasisi za serikali na sekta binafsi imeweza kuunganishwa na inatumika katika uboreshaji wa utoaji wa huduma.” anasema Waziri Kairuki.

“Kwa sasa inakadiriwa idadi ya watu kufikia milioni 70 na majengo yasiyopungua milioni 18 ambayo kati ya hayo takribani majengo milioni 11 ni ya makazi. Ukitazama ukubwa wa nchi yetu; idadi ya majengo na idadi ya watu utaona kuna umuhimu wa kuwa na mifumo imara ya kuweza kutambua makazi ya wananchi.”

Aidha, katika kuboresha mfumo wa NaPa ili kuwa na taarifa sahihi muda wote, waziri Kairuki, amesema mpaka sasa serikali imepata vishikwambi 5,172 kwa watendaji wa kata, mitaa na shehia, ili kuimarisha ukusanyaji na utoaji wa taarifa za wakazi.

Pia, amesema sehemu ya vishikwambi hivyo, 409 vitapelekwa Zanzibar kwa masheha na waratibu wa mfumo, huku vingine 373 vikisambazwa katika halmashauri 23 Tanzania Bara kwa ajili ya kuboresha taarifa za wakazi na usimamizi wa anuani za makazi.

“Nipende kutoa pongezi kwa wizara ya mawasiliano na teknolojia ya habari kwa kufanikisha upatikanaji wa vishikwambi 5,172 kwa ajili ya watendaji wote wa kata, mitaa na shehia licha ya msingi wa uhitaji ni vishikwambi 21,872 ili kukamilisha azma yetu.” amesema Kairuki.

Waziri huyo ametoa rai kwa wadau kujitokeza ili kukamilisha idadi ya vishakwambi vilivyobakia 16,700, hali itakayo ruhusu kila mtendaji wa kata, mtaa au shehia, kuwa na kifaa kitakachorahihisha upatikanaji wa taarifa za anuani za makazi.

Vilevile ameeleza, hatua iliyofikiwa na Tanzania katika kutekeleza na kutumia mfumo wa anuani za makazi, imeendelea kuwa kielelezo cha taifa kuendea uchumi wa kidigitali, kiasi cha kuvutia nchi za jirani kutaka kujifunza namna bora ya kutekeleza mfumo huo katika nchi zao.

Anaongeza kuwa, umuhimu wa mfumo wa anwani za makazi ni kurahishisha eneo la biashara mtandao, ambapo mfumo huo, umeendelea kuleta mageuzi mbalimbali, ikiwamo taarifa sahihi za mahali pakupeleka mzigo jambo ambalo lilikuwa gumu kwa miaka iliyopita.

“Mageuzi haya yametokana na uwezo wa mfumo wa kutoa taarifa za mahali sahihi pakupeleka mzigo. Lakini vile vile tunaamini kupitia matumizi ya mfumo huu, itawezesha kampuni za ndani kuweza kuongeza mauzo ya bidhaa nje.” ameeleza Kairuki.

Katibu Mkuu wa Wizara ya Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Mohammed Khamisi, amesema Maadhimisho ya Kilele cha Wiki ya Anwani za Makazi na Maonesho ya Teknolojia za Posta, yamelenga kuongeza uelewa kwa wananchi kuhusu umuhimu wa mfumo huo.

Amefafanua kuwa, mfumo wa anwani za makazi unamwezesha mwananchi kupata anuani yake binafsi kulingana na mahitaji yake pamoja na kutambua maeneo mbalimbali anayohitaji kuyafikia.

Naima Akida, Mtendaji wa Mtaa wa Ungindoni, Manispaa ya Kigamboni, amesema awali alikuwa akikwama katika utendaji kazi wake, kutokana na mfumo wa NaPa kuhitaji simu maalum, hivyo kupitia ugawaji wa vishikwambi hivyo, itarahisisha utendaji wake ofisini.

Mtendaji huyo anasema zipo shughuli kama; usajili wa barabara mpya, majengo, anuani mpya na kutoa barua za utambulisho kwa wananchi zilishindikana kutokana na mfumo kushindwa kufanya kazi kwenye simu za kawaida

“Ugawaji wa vishikwambi unaenda kurahisisha utendaji wetu kazini, kwa sababu mwanzo mfumo ulikuwa unataka simu maalum, kuna baadhi ya simu hazikubali mfumo wa NaPa. 

Kwa hiyo kupitia upatikanaji wa vifaa hivi, changamoto hizi zitaisha na itasaidia wananchi kupata huduma kwa unafuu.” amesema Naima.