Walalamika mizigo yao kuwasili 'Airport' ikiwa imechomolewa bidhaa.

By Rahma Suleiman , Nipashe
Published at 04:34 PM Feb 10 2026
news
Picha Rahma Suleiman
Walalamika mizigo yao kuwasili 'Airport' ikiwa imechomolewa bidhaa.

MAMLAKA ya Viwanja vya Ndege Zanzibar (ZAA) imekiri kuwepo kwa vitendo vya kuchomolewa bidhaa katika mizigo ya wafanyabiashara katika Uwanja wa Ndege wa kimataifa wa Abeid Amani Karume ikitokea nje ya nchi, ikiwemo Dubai, huku ikishindwa kubaini chanzo cha wizi huo.

Akizungumza na waandishi wa habari, Mkurugenzi wa ZAA, Seif Abdallah Juma, amesema mamlaka ilipokea malalamiko kutoka kwa wafanyabiashara na kufanya vikao na wadau mbalimbali, akiwemo wahudumu wa mizigo, ili kubaini mahali wizi huo unakofanyika.

Amesema uchunguzi wa awali haukuonesha wizi kufanyika ndani ya uwanja huo kwa kuwa kamera za ulinzi zilizopo kuanzia mzigo kushushwa hadi kufikishwa kwenye mkanda wa mizigo hazikuonesha tukio lolote, hali iliyozua dhana kuwa wizi huo huenda unafanyika ndani ya mabehewa ya ndege.

Kutokana na hali hiyo, “mamlaka iliunda kamati maalumu kwa kushirikiana na vyombo vya ulinzi na kuanza kukagua mizigo kabla ya kushushwa pamoja na kuwafanyia ukaguzi wahudumu wa upakuaji, hatua iliyobaini kuwa mizigo mingi ilikuwa tayari imefunguliwa kabla ya kufika Zanzibar.”

Aliongeza kuwa ili kudhibiti tatizo hilo, ZAA iliagiza ndege zote kufunga kamera katika mabehewa ya mizigo na wahudumu kuvaa kamera kwenye vifua vyao, hatua iliyosaidia kukomesha kabisa malalamiko ya wizi wa mizigo kwa wafanyabiashara.