Katibu Mkuu wa Wizara ya Uchukuzi, Profesa Godius Kahyarara, amesema Serikali inaendelea kuwekeza katika Bandari ya Dar es Salaam kufuatia ongezeko la meli kubwa zinazoingia bandarini, hali iliyosababisha kuongezeka kwa shehena ya mizigo.
Akizungumza jijini Dar es Salaam katika kikao cha wadau wa maboresho ya bandari, Prof. Kahyarara amewataka wadau kuchukua mizigo yao kwa wakati ili kutoa nafasi kwa mizigo mingine kuhudumiwa kwa ufanisi. Amehimiza ushirikiano wa karibu kati ya taasisi za Serikali na sekta binafsi, zikiwemo TRA, TPA, TBS, TRC, wamiliki wa malori pamoja na wizara husika.
Ameeleza kuwa uwekezaji unaoendelea unahusisha kuongeza kina cha lango la bahari, ujenzi wa magati, ununuzi wa vifaa na ushirikiano na sekta binafsi, hatua iliyoongeza uwezo wa bandari kuhudumia mizigo.
Kwa upande wake, Meneja wa Bandari ya Dar es Salaam, Abed Gallus, amesema TPA inaendelea kupanua maeneo ya kuhifadhia makasha kutokana na ongezeko la mizigo, ikiwemo kutumia maeneo ya EPZA baada ya ICDs nyingi kujaa.
Naye Meneja wa Uendeshaji wa Shirika la Reli Tanzania (TRC), Focus Sahani, amesema Serikali imenunua vichwa nane vya treni kwa ajili ya kusafirisha makasha kwenda Bandari Kavu ya Kwala, ambapo viwili tayari vinafanya kazi na vingine sita vipo kwenye majaribio.
© 2026 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED