Sharti la lazima kuonesha bei za bidhaa laondolewa

By Augusta Njoji , Nipashe
Published at 11:10 AM Sep 05 2024
   Sharti la lazima kuonesha bei za bidhaa laondolewa
Picha: Mtandao
Sharti la lazima kuonesha bei za bidhaa laondolewa

MUSWADA wa Marekebisho ya Sheria ya Ushindani kwa Mwaka 2024 umepitishwa na Bunge huku likifuta kifungu chenye sharti la lazima la wauzaji bidhaa au huduma kuonesha bei ya kila bidhaa au huduma na kuweka adhabu ya faini isiyopungua Sh. 10,000 na isiyozidi Sh. milioni moja ili kulinda walaji.

Hatua hiyo ilifikiwa baada ya ushauri wa wabunge, ikiwamo kukosa tafsiri ya mfanyabiashara mdogo na hivyo Bunge kushauri kifungu hicho cha 17 kilichoandikwa upya kuweka sharti hilo, kitumike kifungu cha awali kwenye Sheria ya Ushindani ya Mwaka 2023 ambacho hakina sharti la lazima.

 Akifafanua nje ya Bunge baada ya kupitishwa Muswada wa Marekebisho ya Sheria hiyo,  Waziri wa Viwanda na Biashara, Dk. Selemani Jafo, alisema muswada huo ulikuwa na vifungu 24 na hivyo Bunge limepitisha vifungu 23 na hicho kimoja serikali imepewa muda zaidi wa kufanya utafiti na kutafuta tafsiri ya baadhi ya maneno ambayo yataleta utata kwenye utekelezaji wake. 

Waziri Jafo alisema kuwa suala la kuweka bei za bidhaa, Bunge limeshauri kitumike kifungu cha awali na kutumia utaratibu wa mwanzo bila kuweka adhabu na ikiwezekana yafanyike maboresho kwa lengo la kutekeleza sheria kwa ufasaha na wafanyabiashara kuzingatia matakwa ya sheria inavyotaka.

 "Mjadala umekuwa mzuri, tumekuwa na Muswada wa Sheria ya Tume ya Ushindani (FCC) ambao lengo lake lilikuwa kumjali mteja hasa upande wa wamiliki wa hodhi wa soko kutoka asilimia 35 hadi 40," alisema.

 Mkurugenzi Mkuu wa FCC, William Erio, alisema sheria hiyo ni ya muda mrefu na kwamba marekebisho hayo yatawawezesha kufanya kazi kwa ufanisi na kufikia malengo ya serikali ya kuvutia biashara na kumlinda mtumiaji bidhaa au huduma. 

"Marekebisho yaliyofanyika ni mengi, ikiwamo kubadilisha vifungu vya ushindani na kuruhusu tume kutoa adhabu katika makosa yanayomwathiri mlaji ambapo vifungu vingine havikuwapo mwanzo, tunashukuru serikali kwa maboresho haya, yakianza kutumika tutatoa elimu ili watu waelewe zaidi," alisema. 

Juzi wakati wa mjadala bungeni kuhusu muswada huo, wabunge walishauri kifungu hicho kifutwe kwa kuwa kitaumiza wafanyabiashara wadogo, hasa machinga na mama na baba lishe na kushauri kiangaliwe upya.