NMB yavunja rekodi ufanisi kwa mwaka wa fedha 2024

By Mwandishi Wetu , Nipashe
Published at 11:02 AM Jan 31 2025
Afisa Mtendaji Mkuu wa NMB, Ruth Zaipuna.
Picha: Mtandao
Afisa Mtendaji Mkuu wa NMB, Ruth Zaipuna.

Mwaka 2024, Benki ya NMB iliendeleza kasi ya ukuaji, ikipata matokeo ya kipekee ya kifedha na kiutendaji, yaliyochochewa na ukuaji imara wa mizania, ufanisi wa uendeshaji, na umakini mkubwa katika ukopeshaji.

Benki ya NMB ilipata faida kubwa kabla ya kodi kuwahi kupatikana katika historia yake kwa kufikia TZS bilioni 931, ukuaji wa kasi wa 20% ikilinganishwa na TZS bilioni 775 za mwaka wa fedha 2023. Hii ilipelekea kupatikana kwa uwiano wa Faida na Mtaji wa 28%. Ukuaji huu imara wa faida ulitokana na ongezeko la mapato, ufanisi mkubwa wa uendeshaji, na mwendelezo wa kuimarisha ubora wa mikopo. Jumla ya mapato iliongezeka kwa 16% hadi TZS trilioni 1.64, kutokana na ongezeko la Mapato ya Riba Halisi kwa 13% na Mapato Yasiyo ya Riba kwa 23%.

Uwiano wa mapato na matumizi (CIR) uliimarika kwa pointi za asilimia 100 hadi 38%, chini ya ukomo wa kikanuni wa 55%. Maboresho haya yalichangiwa na ufanisi zaidi wa uendeshaji, usimamizi makini wa matumizi, na uwekezaji wa kimkakati kuendeleza rasilimali watu na teknolojia za kidijitali. Hii iliiwezesha benki kuendeleza ukuaji na kuhakikisha ufanisi wa shughuli zake za kifedha.

Aidha, mizania ya Benki iliendelea kukua, huku jumla ya mali ikiongezeka kwa 13% kwa mwaka mzima wa 2024 hadi TZS trilioni 13.7. Mikopo halisi kwa wateja ilikua kwa 10% hadi TZS trilioni 8.5, huku amana zikiongezeka kwa 13% hadi TZS trilioni 9.5. Ukuaji huu thabiti unaakisi dhamira ya NMB katika kuendeleza ujumuishaji wa kifedha, kuboresha huduma kwa wateja na kuendelea kuleta masuluhisho mapya ya kifedha.

Benki pia iliendelea kuimarisha ubora wa mikopo, ambapo uwiano wa mikopo chechefu (NPL) ulipungua hadi 2.9% mwaka 2024 kutoka 3.2% mwaka 2023. Mafanikio haya yalitokana na usimamizi makini wa ukopeshaji na ufuatiliaji wa karibu wa mikopo.

NMB iliendelea pia kuwa na mtaji imara, kutokana na ukuaji wa mapato na ufanisi wa matumizi ya mtaji, hali iliyoiweka benki katika nafasi imara kifedha. Kufikia mwishoni mwa Desemba, Uwiano wa Ufanisi wa Mtaji ulikuwa 23%, kiwango ambacho ni zaidi ya uwiano hitajika kikanuni. Hii inaiweka benki katika nafasi nzuri ya kuongeza uwekezaji, kuzidisha mikopo, na kuendelea kuwa imara kwa muda mrefu.

NMB Yavunja Rekodi na Kuongoza Sekta ya Benki Tanzania

NMB ni benki inayotengeneza faida kubwa zaidi kuliko benki zote Tanzania na imeweka historia ya kuwa benki ya kwanza nchini kufikia thamani ya zaidi ya dola bilioni moja. Mafanikio haya yanathibitisha hadhi ya NMB kama benki kubwa zaidi iliyoorodheshwa katika soko la hisa nchini, benki ya pili kwa ukubwa Afrika Mashariki, na kampuni ya sita kwa ukubwa wa kimtaji katika soko la hisa.

Utendaji thabiti wa kifedha wa NMB unaifanya kuwa miongoni mwa kampuni 30 zenye thamani kubwa katika nchi za Kusini mwa Jangwa la Sahara (SSA) - bila kujumuisha Afrika Kusini. Hii ni kwa mujibu wa Capital Market Union (CMU) katika ripoti yake kuhusu kampuni zinazoongoza katika nchi za SSA.

1

Ubunifu na Uendelevu

Benki ya NMB imethibitisha dhamira yake ya ubunifu na uendelevu. Mwaka 2024, benki iliorodhesha kwa mara ya kwanza hati fungani endelevu ya NMB Jamii Bond, ambayo ni ya kwanza ya aina hiyo Kusini mwa Jangwa la Sahara, katika Soko la Hisa la London (London Stock Exchange) na Soko la Hisa la Luxembourg (Luxembourg Stock Exchange). Katika muktadha huo, NMB iliwekeza zaidi ya TZS bilioni 5.4 katika sekta za elimu, afya, na miradi inayohusiana na mabadiliko ya tabianchi, ikiimarisha dhamira yake ya kuchangia ustawi wa jamii na kuhifadhi mazingira.

Mafanikio haya yanaonesha umakini wa benki katika ufanisi wa utekelezaji wa mikakati yake, ukuaji, ubunifu, na uendelevu, na kuthibitisha nafasi yake kama kiongozi katika sekta ya benki kwenye ukanda huu.

Kauli ya Afisa Mtendaji Mkuu wa NMB

Akizungumzia matokeo na ufanisi huu, Afisa Mtendaji Mkuu wa NMB, Ruth Zaipuna, alisema: "Mwaka 2024 umekuwa wa kipekee kwa Benki ya NMB, ukiwa wa mafanikio makubwa ya kifedha na utendaji, ukuaji wa kimkakati, na mchango mkubwa katika maendeleo ya uchumi wa Tanzania. Matokeo haya yanaonyesha uimara wa tulivyojipanga kibiashara, kujitolea kwa wafanyakazi wetu, na uaminifu wa wateja wetu. Katika siku zijazo, tutaendelea kuhamasisha na kukuza ubunifu, kupanua huduma jumuishi za kifedha, na kutoa thamani endelevu kwa wadau wetu wote."

Matarajio na Mwelekeo wa Mwaka 2025

Benki ya NMB imejipanga vizuri kuendeleza mafanikio yake mwaka 2025, ikiwa na mkakati thabiti unaolenga ukuaji, ubunifu, na uendelevu. Benki itaendelea kuwekeza katika teknolojia, vipaji, na masuluhisho yanayomlenga mteja ili kuendeleza ujumuishi wa kifedha na kuchangia maendeleo ya uchumi wa Tanzania. NMB itaendeleza dhamira yake ya kudumisha uwezo wake mkubwa kifedha, kuwapa thamani wanahisa wake, na kuchangia ustawi na maendeleo ya jamii inazohudumia.