NMB yatenga milioni 450/- za kuhamasisha malipo kwa kadi

By Mwandishi Wetu , Nipashe
Published at 01:01 PM Nov 11 2024
NMB yatenga milioni 450/- za  kuhamasisha malipo kwa kadi
Picha:Mpigapicha Wetu
NMB yatenga milioni 450/- za kuhamasisha malipo kwa kadi

BENKI ya NMB imezindua msimu wa sita wa kampeni maalumu ya kuhamasisha matumizi na malipo kwa njia ya kadi ‘NMB MastaBata - La Kibabe,’ ambayo kwa miezi mitatu mfululizo wateja wa benki hiyo watajishindia zawadi zenye thamani ya zaidi ya Sh. milioni 300, pamoja na safari za utalii wa ndani na nje ya nchi.

NMB MastaBata ni kampeni iliyoanza mwaka 2018, kabla ya kuboreshwa zaidi mwaka 2019 ilipoitwa MastaBata ‘Sio Kawaida,’ ikafuata MastaBata ‘KivyakoVyako’ mwaka 2020, kabla ya mwaka 2021 kuitwa Mastabata ‘Kotekote,’ na mwaka jana kutambuliwa kama Mastabata ‘Halipoi.’

Uzinduzi huo uliosimamiwa na Ofisa wa Bodi ya Michezo ya Kubahatisha Tanzania (GBT), Rasul Masoud, ulifanyika Mlimani City, Dar es Salaam juzi na kampeni hiyo itadumu hadi Februari 12 mwakani, siku ambayo washindi sita wa fainali na wenza wao watapatikana kwa safari ya Dubai kwa siku tano iliyogharamiwa na NMB.

Katika kipindi hicho, droo mbalimbali zitachezeshwa, ambako washindi 100 wa kila wiki watapokea Sh. 100,000 katika akaunti zao, huku washindi 30 wakijinyakulia Sh. 500,000 kila mwisho wa mwezi kwa miezi miwili na wengine 10 wakijishindia safari ya kwenda kutembelea Mbuga za Wanyama za Mikumi na Ngorongoro.

Kwa miaka sita, NMB imejikita katika kuhamasisha wateja wao wenye kadi za benki hiyo, kufanya malipo ya bidhaa, hotelini, migahawani, ‘supermarket,’ maeneo ya starehe na popote pale, huku ikitenga kitita cha fedha taslimu kama zawadi, bidhaa za zawadi na safari za kitalii ndani na nje ya nchi.

Mkuu wa Idara ya Kadi ya Benki ya NMB, Philbert Casmir, alisema kampeni hiyo itayofikia ukomo Februari 12 mwakani, ni kwa ajili ya wateja wenye kadi za NMB Mastercard, ama kadi ya aina yoyote inayotolewa na benki hiyo, huku akiwataka wasio na akaunti na kadi za NMB, kufungua sasa kampeni inapoendelea.

"Washindi zaidi ya 2,000 watapata nafasi ya kujishindia zawadi mbalimbali zenye thamani ya zaidi ya Sh. milioni 450, ambapo ili kushiriki kampeni hii utatakiwa kufanya ununuzi kwa kutumia kadi yako ya NMB Mastacard kwenye mashine za POS, kwenye mitandao (online) na Lipa kwa QR link. 

"Katika kuhitimisha kampeni hii, washindi sita watajishindia tiketi za kwenda Dubai pamoja na wenza wao kwa siku tano, safari itakayogharamiwa kila kitu na NMB," alisema Casmir huku akibainsiha ununuzi huo utakaofanyika kwenye migahawa, ‘supermarket,’ vituo vya mafuta, maduka makubwa na sehemu za starehe.

"Faida za matumizi kwa njia ya kadi nyingi na tunatamani kuona kila mteja wetu ananufaika nayo, ambazo ni pamoja na urahisi wa kutumia bila kuwa na fedha taslimu mkononi, ambazo ni hatari kutembea nazo. Lakini hii inakupa fursa ya kuweka rekodi za matumizi ya fedha zilizomo katika akaunti," alibainisha Casmir.

Akizungumza katrika uzinduzi huo, Ofisa Mkuu wa Wateja Binafsi na Biashara wa NMB, Filbert Mponzi, aliwataka watanzania kujitokeza kwa wingi kufungua akaunti ili kunufaika na huduma za NMB, zikiwamo promosheni mbalimbali zinazoendelea. 

"NMB tunazo kampeni zinazowapa zawadi wateja wapya wanaofungua, kuna kampeni inayotoa zawadi kwa wateja wenye akiba isiyopungua Sh. 100,000, na leo tunakuletea kampeni hii ambayo inakuwazawadia unapotumia fedha zako kwa njia ya kadi tu, pale utapofanya ununuzi kwenye mashine za PoS au NMB Pay by Link.

"Hii maana yake utafanya ununuzi wa bidhaa zako, na kukupeleka kwa safari za utalii wa ndani na nje ya nchi, na unaweza kujikuta ukishinda zawadi ya ada ya shule ya mtoto wako inayofikia Sh. milioni nne, ambazo zitakwenda kwa washindi wetu 10," alibainisha Mponzi. 

Mponzi alibainisha kuwa katika droo za kila mwezi, washindi 10 watakaopatikana, watagawanywa makundi ya washindi watano watakaokwenda Mikumi na Ngorongoro kwa gharama za NMB, kama itakavyokuwa kwa washindi sita wa fainali na wenza wao, watakaopelekwa Dubai kwa siku tano. 

8