MBUNGE wa Jimbo la Ndanda (CCM), Cecil Mwambe, ametoa mitungi 160 ya majiko ya gesi ya kilo sita kwa viongozi wa Jumuiya ya Umoja wa Wazazi, Wanawake (UWT) na Umoja wa Vijana (UVCCM) wa jimbo la hilo.
Lengo likiwa ni kuhamasisha jamii kujikita katika matumizi ya nishati safi.
Akiongea katika mafunzo ya itikadi na uongozi kwa viongozi hao Jumuiya za CCM kutoka kata za Jimbo la Ndanda, mafunzo ambayo yamefanyika katika ukumbi wa jengo la zamani la halmashauri ya wilaya ya Masasi mkoani Mtwara, alisema lengo ni kuunga mkono ajenda ya serikali kupiga vita mabadiliko ya tabianchi na uchafuzi wa mazingira.
Alisema matumizi ya nishati safi ya kupikia yatasaidia kutunza mazingira na uchafu wa mazingira na viongozi hao kwa sasa hawapaswi kutumia mkaa na kuni kwa kutunza mazingira.
Mwambe alisema viongozi hao ni muhimu katika ngazi ya kata na yeye ataendelea kushirikiana vema na jumuiya hizo katika kuleta maendeleo katika Jimbo la Ndanda.
"Natumia fursa hii kumpongeza Rais Dk. Samia Suhulu Hassan kwa kutoa fedha nyingi za miradi ya maendeleo katika Jimbo la Ndanda na tutaungana naye katika kuhifadhi na kutunza mazingira," alisema Mwambe.
Pia viongozi hao wa Jumuiya za CCM wamepatiwa mafunzo ya itikadi na uongozi ili kuwajengea uwezo wa kiutendaji katika majukumu yao.
Aliwataka viongozi hao kuendelea kushikamana pamoja ili kudumisha umoja ndani ya chama ili kupata maendeleo kwa rahisi zaidi.
Mmoja wa wanufaika wa msaada huo, Schristina Bakari, akiongea kwa niaba ya wenzake alisema jiko hilo linakwenda kumwongezea tija katika upishi wake wa chakula na kuhudumia wateja wake.
"Kwa kutumia jiko hili litanifanya nisinunue kuni kwa ajili ya kupikia ambapo kipindi cha mvua kama hiki kuna wakati tunanunua kuni zikiwa zimenyeshewa wakati wa kusafirishwa na kutusumbua wakati wa kupika, nawashukuru Taifa Gas kwa kututhamini sisi wanawake," alisema.
© 2024 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED