Kamati ya yabaini shida kampuni za bima nchini

By Augusta Njoji , Nipashe
Published at 08:08 AM Feb 14 2025
Mwenyekiti wa PAC, Naghenjwa Kaboyoka.
Picha: Mtandao
Mwenyekiti wa PAC, Naghenjwa Kaboyoka.

KAMATI ya Bunge ya Hesabu za Serikali (PAC) imebaini kuwapo changamoto katika usimamizi wa watoa huduma za bima nchini na ufuatiliaji madhubuti wa utendaji wa kampuni za bima.

Mwenyekiti wa PAC, Naghenjwa Kaboyoka aliyasema hayo bungeni jana alipowasilisha taarifa ya mwaka ya shughuli za kamati hiyo.

Alisema changamoto za usimamizi zimesababisha kutokutolewa huduma bora za bima ambazo zinatarajiwa kutolewa na kampuni za bima na kuwapo ucheleweshaji malipo ya fidia kwa wateja wa huduma za bima pindi wanapopata majanga.

Kaboyoka alisema uchambuzi wa kamati umebainisha hoja kadhaa ambazo zinatakiwa kufanyiwa kazi na serikali kuhakikisha thamani halisi ya fedha za umma na maslahi ya wananchi inapatikana katika sekta ya bima.

Alisema maeneo hayo ni pamoja na ongezeko la asilimia 11 la madai ya bima yanayodaiwa kwa kampuni za bima.

“Taarifa ya ukaguzi imebainisha kuwapo ukiukwaji Sheria ya Bima ya Mwaka 2009 Sura 394 katika Kifungu cha 131(1) kinachohitaji kila kampuni ya bima kulipa madai ndani ya siku 40 toka tarehe ya kutiwa saini hati ya malipo.

"Endapo kampuni itashindwa kulipa madai ndani ya muda huo, inaweza kuomba kwa Kamishna wa Bima kuongezwa muda, na kamishna anaweza kutoa muda wa ziada usiozidi siku 45 mpaka madai hayo kukamilika," alisema.

Pia alisema TIRA haikuandaa na kutekeleza mpango wa uhamasishaji kuhusu masuala ya bima kupitia mitandao ya kijamii kati ya mwaka wa fedha 2019/20 na 2022/23.

"Hali hii ilipunguza uelewa wa umma, ushirikishwaji wadau na utoaji taarifa za usimamizi wa huduma za bima nchini. Ingawa mpango huo uliidhinishwa Desemba 2023, utekelezaji wake bado ulikuwa katika hatua za awali katika kipindi cha mwezi Desemba mwaka 2024," alisema.

Kaboyoka alisema kuna dosari katika kusimamia ushughulikiaji malalamiko yanayotokana na madai ya bima yasiyolipwa na moja ya changamoto ni mwingiliano wa majukumu kati ya TIRA na Msuluhishi wa Migogoro ya Bima (TIO).

"Ukaguzi pia ulibaini kuwa TIRA ilikuwa ikijihusisha na shughuli za kushughulikia malalamiko nje ya mamlaka yake. Ripoti ya utekelezaji ya TIRA ya mwaka wa fedha 2020/21 ilibainisha kuwa mamlaka hiyo ilipokea na kutatua malalamiko moja kwa moja kutoka kwa wateja wa bima, kinyume cha masharti ya vifungu vya 122 na 123 vya Sheria ya Bima na Kanuni ya (6) ya Msuluhishi wa Migogoro ya Bima," alisema.

Mwenyekiti huyo alisema hatua hiyo imesababisha ucheleweshaji katika kulipa wateja wa bima kwa haki na kwa wakati, na pia kukwamisha uelewa wao wa ofisi inayostahili kushughulikia malalamiko yao.

Pamoja na hayo alisema kampuni za bima hazikuwa zinaweka ipasavyo dhamana inayotakiwa kisheria katika Benki Kuu ya Tanzania.

"Kanuni hiyo inataka kampuni za bima kuweka na kudumisha amana ya dhamana ya angalau asilimia 50 ya kiwango cha chini cha mtaji ulioko Benki Kuu ya Tanzania. Amana hiyo inapaswa kuwa sehemu ya mali kuhusiana na mtaji wa kampuni husika," alisema.

Kuhusu ukwasi wa kampuni za bima kuwa chini ya kiwango cha kisheria, Kaboyoka alisema Ofisa Masuuli aliifahamisha kamati kuwa ni sahihi. Kuna kampuni za bima sita ambazo ukwasi wake ulikuwa chini ya kiwango kinachotakiwa kisheria kwa maana ya Sh. bilioni 2.5 kwa kampuni ya bima ya kawaida na Sh. bilioni tisa.

"Ofisa Masuuli TIRA aliifahamisha kamati kuwa, hatua ya mwisho kwa mujibu wa sheria ambayo TIRA inaweza kuchukua dhidi ya kampuni za bima zenye ukwasi mdogo na zilizokiuka taratibu ni kufunga kampuni endapo TIRA itajiridhisha kuwa kampuni hizo zina changamoto za ukwasi na za kiutendaji kwa mujibu wa sheria," alisema.

Akichangia taarifa ya kamati hiyo, Mbunge wa Vwawa (CCM), Japhet Hasunga, alipendekeza Bunge litenge muda wa kutosha kuhakikisha kila taasisi inayoguswa na ripoti ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) ili kamati ipate kuzipitia na kupeleka mapendekezo yake bungeni na kushauri serikali kuboresha utendaji kazi na kutekeleza matakwa ya utawala bora.