Dar yazalisha taka tani 4.5 kwa siku

By Joseph Mwendapole , Nipashe
Published at 06:42 AM Sep 22 2024
Mkurugenzi wa Kurugenzi ya Uzingatiaji na Utekelezaji Sheria katika Baraza la Taifa la Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira (NEMC), Hamad Taimur.
Picha: NEMC
Mkurugenzi wa Kurugenzi ya Uzingatiaji na Utekelezaji Sheria katika Baraza la Taifa la Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira (NEMC), Hamad Taimur.

TAKWIMU zinaonesha kuwa licha ya Jiji la Dar es Salaam kuzalisha taka ngumu tani 4.5 kwa siku, ni asilimia 6.5 tu ya taka hizo zinazorejelezwa kuwa bidhaa mbalimbali.

Hayo yalibainishwa juzi na Kaimu Mkurugenzi wa Kurugenzi ya Uzingatiaji na Utekelezaji Sheria katika Baraza la Taifa la Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira (NEMC), Hamad Taimur, wakati wa mafunzo kwa waandishi wa habari kuhusu uhifadhi wa mazingira.

Alisema Wilaya ya Temeke inaongoza kwa kuzalisha tani 1,494 za taka kwa siku, ikifuatwa na Ilala inayozalisha taka tani 1,320, Kinondoni tani 982, Ubungo tani 828 na Kigamboni tani 228.

Alitaja aina ya taka zinazorejelezwa kuwa ni plastiki, karatasi, vyuma chakavu, makopo ya alminium, kioo na taka zinazooza.

Alisema kiasi cha taka oza  zinazorejelezwa katika Jiji la Dar es Salaam ni tani 8.9 kwa mwezi ambapo tani 3,800 hurejelezwa katika kituo cha Bonyokwa, tani 3,200 Vingunguti, tani 1,500 katika kituo cha Mabwepande pamoja na vituo vingine.

Alisema serikali imekuwa inaandaa miongozi ya udhibiti wa taka ngumu kwa kutumia dhana ya Punguza, Tumia Tena na Rejeleza.

Alisema serikali kwa kushirikiana na wadau imewezesha kujengwa vituo vya kuchakata na uchambuzi wa taka ngumu na inafanya mapitio ya Kanuni za Usimamizi na Udhibiti wa Taka Ngumu za Mwaka 2024.

Alisema serikali imeendelea kujengea uwezo wa viongozi na wataalamu katika ngazi za wizara, mikoa na Mamlaka za Serikali za Mitaa katika kuwawezesha kuboresha mifumo ya usimamizi wa taka ngumu.

Kuhusu changamoto, alisema kuna shida ya uelewa na mwitikio mdogo wa wananchi kuhusu namna ya kutenganisha taka katika ngazi ya kaya pamoja na uhaba wa miundombinu stahiki kuwezesha utenganishaji taka.

Alisema hali hiyo husababisha kuongezeka kwa wingi kwa taka zinazotupwa katika madampo licha ya kwamba zingeweza kurejelezwa na kuwa bidhaa zingine.

Alitaja changamoto nyingine ni uhaba wa miundombinu stahiki ya udhibiti wa taka ngumu ambazo ni pamoja na miundombinu ya kuhifadhi, kutenganisha, uondoshaji, usafirishaji na utupaji taka.

Alisema kumekuwa na uzingatiaji hafifu wa mipango miji inayosababisha kuwapo ujenzi wa makazi yasiyozingatia mipango husika na hivyo kuchangia kuwapo changamoto katika ukusanyaji taka zinazoweza kurejelezwa.

"Kumekuwa na mwamko hafifu wa matumizi ya mbolea itokanayo na taka na kusababisha mahitaji hafifu ya mbolea zitokanazo na taka zinazooza kwa jamii hususani kwa wakulima," alisema.

Ofisa huyo alisema serikali inaendelea kuchukua hatua madhubuti ili kuboresha usimamizi wa taka ngumu na kukabiliwa na ongezeko kubwa la uzalishaji taka ngumu unaotokana na ongezeko la watu, shughuli za kiuchumi na ukuaji wa miji.

"Tukumbuke kuwa kila mmoja wetu ana jukumu kubwa la kulinda na kuyatunza mazingira kwa ajili ya ustawi na maendeleo ya nchi yetu kwa faida ya kizazi cha sasa na vizazi vijavyo, tusidhani mazingira ni jukumu la watu fulani," alisema.