WAJUMBE wa Baraza la Taifa la Mashirika yasiyo ya Kiserikali (NACoNGO) na Wasajili Wasaidizi wametakiwa kusimamia ipasavyo uratibu, usajili na ufuatiliaji wa shughuli za Mashirika hayo katika mamlaka za Mikoa na Serikali za Mitaa ili kuongeza uwazi, uwajibikaji na kuzingatia mila na desturi za mtanzania.
Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum, Felister Mdemu ametoa kauli hiyo alipokuwa akifungua mafunzo kwa wajumbe hao jijini Dodoma.
Amesema kanzi data inaonesha kuna mashirika 9,776 ambayo yanafanya kazi kwenye sekta mbalimbali na ili kurahisisha uratibu, Baraza hilo na Wasajili wasaidizi ni vyombo muhimu katika kuratibu usajili na kufuatilia shughuli zinazofanywa na Mashirika kwenye Mamlaka za Mikoa na Serikali za Mitaa.
“Hivyo, baada ya mafunzo haya tunategemea kutakuwa na ongezeko la Mashirika kufuata Sheria na kanuni hasa katika utumaji wa taarifa za utekelezaji na ulipaji wa ada,”amesema.
Amebainisha Wizara inatambua kuwa kuna changamoto mbalimbali katika uratibu kama vile, ukosefu wa mafunzo ya mara kwa mara kuhusu sheria, kanuni na miongozo ya mashirika, mafunzo ya mfumo wa Kieletroniki wa usajili na uratibu (NIS), na ufinyu wa bajeti ya kufanya ufuatiliaji wa shughuli zao.
© 2025 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED