Yanga kutikisa nchi

By Somoe Ng'itu , Nipashe Jumapili
Published at 09:25 AM Jun 09 2024
Ofisa Habari wa Yanga, Ali Kamwe.
Picha: Mtandao
Ofisa Habari wa Yanga, Ali Kamwe.

MBALI na kutambulisha makombe iliyotwaa katika msimu uliomalizika, Yanga inajipanga kuwapa 'sapraizi' mashabiki wake katika mkutano mkuu wa wanachama utakaofanyika leo kwenye Ukumbi wa Kimataifa wa Julius Nyerere (JNICC) jijini, Dar es Salaam.

Yanga ikiwa chini ya Kocha Mkuu, Miguel Gamondi, imetetea taji la Ligi Kuu Tanzania Bara, Kombe la FA na kucheza hatua ya robo fainali ya mashindano ya kimataifa ya Ligi ya Mabingwa Afrika.

Ofisa Habari wa Yanga, Ali Kamwe, alisema maandalizi kuelekea mkutano huo yamekamilika na kwa wakati mwingine muhimu wanatarajia kuelezea mikakati ya klabu kwa ajili ya msimu mpya wa mashindano.

Kamwe alisema mkutano huo unafanyika kwa mujibu ya katiba yao na amewaomba viongozi wa matawi wanaotambulika kuhudhuria bila kukosa.

"Tuko katika kumalizia maandalizi ya mkutano wetu utakaofanyika kesho (leo), hata hivyo hawaruhusiwi wanachama wote, ni wale viongozi ambao katiba inawatambua, ni viongozi watano kutoka katika kila tawi lililopo duniani kote ambapo Yanga inapatikana," alisema Kamwe.

Aliongeza mkutano huo utaongozwa na Rais, Hersi Said, na hii imekuwa ni utaratibu wa Yanga kukutana baada ya kumalizika kwa msimu.

"Ni nafasi nzuri ya kuwaambia  wanachama namna msimu ulivyokuwa na yale ambayo walimwagiza (Rais), kuona utekelezaji wake, lakini ni sehemu ya kupanga mikakati kuelekea msimu mpya wa mashindano. 

Katika mikutano yetu kila mwaka tunakuwa na 'sapraizi' sasa wanachama wanatakiwa kuja kwa wingi, na kufuatilia kuangalia safari hii tutawaletea nini," ofisa huyo alisema.

Naye Hersi alisema mkutano huo utakuwa na ajenda mbalimbali ikiwamo kuthibitisha hesabu za fedha zilizokaguliwa pamoja na kuwasilisha hesabu za mapato na matumizi ya klabu yao.

Hersi alisema wanaahidi wataendelea kuimarisha kikosi chao kwa kusajili wachezaji bora na wenye uzoefu watakaosaidia timu yao kufanya vizuri katika mashindano yote watakayoshiriki.