Prisons yamsajili nyota wa zamani Simba

By Adam Fungamwango , Nipashe Jumapili
Published at 04:12 PM Jul 14 2024
 Haruna Chanongo.
Picha: Maktaba
Haruna Chanongo.

KLABU ya Prisons imefanikiwa kunasa saini ya winga wa zamani wa Simba na timu ya taifa ya Tanzania, Taifa Stars, Haruna Chanongo.

Mchezaji huyo amejiunga na kikosi hicho akitokea Pamba FC, ambapo alikuwa mmoja wa wachezaji tegemeo walioisaidia timu hiyo kupanda daraja kutokea Ligi ya 'Championship'.

Uongozi wa klabu hiyo ulithibitisha usajili huo jana kupitia taarifa yao rasmi ya klabu hiyo.

"Karibu kwenye familia ya wajelajela kiungo na winga, Chanongo, kuanzia leo ni mali ya Prisons," ilisema taarifa rasmi ya klabu hiyo jana.

Klabu hiyo imemsajili winga huyo mzoefu kwenye Ligi Kuu ya Tanzania Bara ili kukiimarisha kikosi chake kuelekea msimu ujao  baada ya kulazimika kupambana sana kubakia Ligi Kuu msimu uliopita.

Chanongo alikuwa mmoja wa wachezaji waliopandishwa kwenye kikosi cha kwanza cha Simba kutoka kikosi cha pili cha timu hiyo mwaka 2012.

Aliichezea Simba hadi mwaka 2015 na kutimkia Stand United, hadi 2016 alipojiunga na Mtibwa Sugar ambapo aliichezea timu hiyo hadi mwaka 2022 alipokwenda Ruvu Shooting na msimu uliofuata akaenda kuichezea Pamba FC ikiwa 'Championship'.

Klabu hiyo pia imemsajili golikipa wa Geita Gold, Sebusebu Samson kwa ajili ya kuongeza nguvu eneo hilo.

Sebusebu ni mmoja wa magolikipa mahiri, ambaye alifungwa mabao machache kwenye Ligi Kuu licha ya timu yake ya Geita Gold kushuka daraja.