Kocha Fadlu ataka Simba itakayofunga mabao mengi

By Adam Fungamwango , Nipashe Jumapili
Published at 04:07 PM Jul 14 2024
Kocha Mkuu wa Simba, Fadlur Davids.
Picha: Simba
Kocha Mkuu wa Simba, Fadlur Davids.

KOCHA Mkuu wa Simba, Fadlur Davids, ameahidi kusuka safu kali ya ushambuliaji itakayokuwa tishio kwa timu yoyote itakayokutana nayo akitaka washambuliaji wake wafunge mabao mengi katika mechi moja.

Akizungumza jana kutoka Ismailia nchini Misri ambako kikosi cha Simba kimeweka kambi, amesema moja ya kazi ambayo ataifanya ni kutengeneza safu kali ya ushambuliaji kwa sababu kwake ni kazi rahisi kwani katika karia yake ya soka alikuwa mshambuliaji na amewahi kuwa mfungaji bora mara mbili nchini Afrika Kusini wakati akicheza soka.

Kocha huyo maarufu Afrika Kusini, ndiyo kwanza ameanza kukinoa kikosi cha Simba kuelekea msimu ujao wa mashindano, akichukua mikoba ya Abdelhak Benchikha raia wa Algeria aliyeondoka kabla ya Ligi Kuu ya msimu uliopita kumalizika.

"Nataka kutengeneza safu kali ya ushambuliaji, tunatakiwa kufunga mabao mengi ili kushinda mchezo wa mpira wa miguu, usipofunga utatoa sare, au utafungwa kabisa, ninachofanya ni kutengeneza muunganiko, maelewano, mikimbio ya kusaka nafasi, mawasiliano ya mdomo na mwili kwa washambuliaji wangu ili wafunge mabao mengi kama nilivyokuwa nafunga mimi, hata kuwafua vyema wale wanaotengeneza nafasi, viungo washambuliaji ambao nao watatakiwa kuwa na maelewano, kutengeneza mfumo wa kucheza kwa kuwahadaa mabeki, au kupiga mipira juu ya migongo yao ili kulisha washambuliaji ili wafunge kwa urahisi," alisema kocha huyo.

Hata hivyo, alisema hayo yote hayawezi kufanyika bila ya kuwa na msingi imara wa mabeki na viungo wakabaji ambao wana uwezo mzuri na kupora mipira wapinzani mara tu wanapoipoteza.

Akizungumzia siku za awali za mazoezi, alisema walikuwa na kazi kubwa kwanza ya kuzoea hali ya hewa na kufahamiana baina ya makocha na wachezaji.

"Kwanza tulikuwa na kazi ya kuzoea hali ya hewa, makocha wangu wa utimamu wa mwili wakaanza kufanya kazi, tulijaribu kuwazoea wachezaji na wao kutuzoea sisi, kikubwa nilitaka kujua aina ya wachezaji ninaofanya nao kazi, hii ndiyo hali tuliyokutana nayo siku za mwanzo, kidogo kidogo wataanza kupokea na kuyafanyia kazi maelekezo na mafundisho tunayowapa," alisema Fadlu.

Aliwataka wanachama na mashabiki wa Simba kujitokeza kwa wingi katika tamasha la 'Simba Day' ili waje kuona makocha na wachezaji wao wapya, pamoja na soka safi la kuvutia.

"Nawaomba wanachana mashabiki waje kutuona kwa mara ya kwanza, ni siku ya utambulisho wa benchi la ufundi ambalo ni jipya na wachezaji wao wa msimu ujao wakiwemo waliosajiliwa hivi karibuni,  lakini pia waje kuona soka safi," alisema kocha Fadlu.