Gamondi: Nataka kuifanya Yanga iwe tano bora Afrika

By Mwandishi Wetu , Nipashe Jumapili
Published at 04:03 PM Jul 14 2024
KOCHA Mkuu wa Yanga, Miguel Gamondi akiwaonesha jambo wachezaji wa Yanga wakiwa mazoezini.
Picha: Mtandao
KOCHA Mkuu wa Yanga, Miguel Gamondi akiwaonesha jambo wachezaji wa Yanga wakiwa mazoezini.

KOCHA Mkuu wa Yanga, Miguel Gamondi amesema anataka kutengeneza kikosi tishio zaidi kuliko cha msimu uliopita, huku lengo lake ikiwa ni kuifanya timu hiyo iingie kwenye timu tano bora Afrika.

Akizungumza jana jijini Dar es Salaam, kocha huyo raia wa Argentina, aliyeiwezesha Yanga kutwaa ubingwa wa Tanzania Bara msimu uliopita na kufika hatua ya robo fainali ya Ligi ya Mabingwa Afrika, alisema pamoja na matamanio hayo bado wanatakiwa kufanya kazi ya ziada kufikia malengo hayo.

Alisema malengo hayo yanaweza kufanikiwa kutokana na kuongeza baadhi ya wachezaji wenye viwango vikubwa kwenye usajili.

"Kila mtu anajua aina yangu ya ufundishaji ni kucheza soka la kuvutia, kupata ushindi na mataji, lakini kuelekea msimu ujao tunataka kuwa bora zaidi kuliko msimu uliopita ingawa haitokuwa rahisi, kutakuwa na changamoto kubwa, huu ni ujumbe kwa mashabiki wote wa Yanga na wadau wa soka kuendelea kutuunga mkono msimu ujao, ya msimu uliopita yamepita, wajue msimu ujao tutapata changamoto kutokana na uwezo wetu mkubwa tuliokuwa nao huko nyuma, hivyo timu nyingi zitakuwa zimejiandaa kwa kusajili vizuri na kutengeneza nguvu ya kupambana na sisi, hivyo sisi tunatakiwa tuongeze ubora zaidi," alisema kocha huyo.

Alisema pamoja na kwamba watakutana na ugumu, lakini na wao watakabiliana nao kwani wameongeza baadhi ya wachezaji wachache ambao wana uwezo wa hali ya juu hasa kwenye michuano ya kimataifa.

"Hatukutaka wachezaji wengi ndani ya kikosi chetu, bali wachache tu wenye ubora wa kutuongezea nguvu, tulitaka wale wazoefu wa michuano ya Ligi ya Mabingwa Afrika lengo ni kuendelea kutawala soka la Tanzania na kufanya vyema zaidi ya msimu uliopita kwenye michuano ya kimataifa, hii ni ngumu, ila nataka Yanga iwe ndani tano bora katika bara la Afrika na hili litatokana na ushirikiano wa Wanayanga wote, nasema najua ni ngumu kwa sababu huwezi kushinda kila mechi, lakini angalau kurudia matokeo tuliyoyapata huko nyuma karibuni kila msimu, ni vyema sana na inaweza kutufikisha huko," alisema Gamondi.

Yanga kwa sasa inashika nafasi ya 13 kwenye ubora barani Afrika, kwa mujibu wa Shirikisho la Mpira wa Miguu barani Afrika (CAF) wakiwa na pointi 31, huku watani wa jadi Simba wakiwa kwenye nafasi ya saba kwa kujikusanyia pointi 39.

Kikosi hicho kwa sasa kipo mazoezini Kigamboni kikijiandaa na msimu mpya huku kikiwa kimewaongeza wachezaji kadhaa akiwemo Mzambia Clatous Chama aliyekuwa mchezaji wa Simba, Mzimbabwe Prince Dube aliyesajiliwa kutoka Azam FC, Mkenya, Duke Abuya na golikipa Mtanzania, Khomeiny Aboubakar, wote kutoka Singida Black Stars na Mkongomani Shadrack Boka kutoka FC Saint Eloi Lupopo kutoka DR Congo.