Cadena aanika siri Simba kichapo 5-1

By Adam Fungamwango , Nipashe Jumapili
Published at 09:22 AM Jun 09 2024
Kocha wa Makipa wa Simba, Daniel Cadena.
Picha: Mtandao
Kocha wa Makipa wa Simba, Daniel Cadena.

IKIWA zimepita siku chache msimu wa Ligi Kuu Tanzania Bara 2023/2024 kumalizika, Kocha wa Makipa wa Simba, Daniel Cadena, amefichua sababu iliyopelekea timu hiyo kupokea kichapo cha aibu cha mabao 5-1 kutoka kwa watani zao, Yanga ilitokana na shinikizo la kupangwa langoni, Aishi Manula.

Manula aliyekuwa majeruhi alisimama langoni Novemba 5, mwaka jana kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa na kufungwa idadi hiyo ya mabao.

Akizungumza na gazeti hili jana, Cadena, ambaye hana uhakika wa kuendelea na kibarua chake alisema shinikizo kutoka kwa baadhi ya viongozi lililazimisha Manula kupangwa wakati yeye alipendekeza kipa mwingine.

Cadena alisema ili Simba irejee katika ushindani, mabosi wanatakiwa kufanya mabadiliko 'makubwa' katika kila idara hasa kwa kuwaondoa watu ambao wamedumu kwa muda mrefu klabuni hapo.

Kocha huyo alisema 'watu' wakifanya kazi sehemu moja kwa muda mrefu huwa na tabia ya kuridhika.

Alisema kuelekea katika mchezo huo alikataa Manula asidake lakini ilitolewa amri kutoka 'juu' ikisema ni lazima kipa huyo adake na akaambiwa yupo tayari kwa mchezo, ingawa yeye (Cadena),  alimfuata kipa huyo faragha na kumtaka asikubaliane na uamuzi huo.

"Najua uwezo wa makipa wangu, kabla ya mechi kocha mkuu huwa ananiuliza maoni yangu lakini kabla ya kucheza na Yanga hakuniuliza, alitoa amri tu, lakini pamoja na hayo nikamfuata Manula na kumwambia hatakiwi kucheza kutokana na hali ya kiafya, kilichotokea baada ya mechi matokeo yakawa tumefungwa 5-1," alisema kocha huyo.

Alishauri ili Simba ifanye katika msimu ujao, inatakiwa kutooneana 'aibu' na badala yake itafute watu wengine wenye weledi na uzoefu.

"Endapo kama  watataka kufanikiwa inabidi wasafishe kila eneo kwa kuwaondoa watu ambao wamedumu ndani ya klabu kwa muda mrefu, unajua watu wakifanya kazi sehemu moja kwa muda mrefu huwa wanaridhika na hilo limeliona ndani ya klabu na kikosi," alisema kocha huyo aliyejiunga na Simba akitokea Azam FC.

Kufunguka kwa kocha huyo kumezidi kukoleza moto kwenye petroli, kwa sababu tayari 'joto limepanda' kufuatia Mwekezaji na Rais wa Heshima wa Simba, Mohamed Dewji 'Mo Dewji' kuwataka Wajumbe wa Bodi wa upande wake kujiuzulu ili kupisha mabadiliko, tayari baadhi wametii maombi hayo.

Taarifa zaidi kutoka kwa mwekezaji huyo zinasema ameamua kushiriki moja kwa moja katika kusuka kikosi imara uamuzi ambao anaamini utajenga timu yenye ushindani kama ilivyokuwa miaka ya nyuma.

Chanzo chetu kinasema Mo Dewji amewarejesha katika utendaji vigogo waliowahi kufanya vyema kuanzia zoezi la usajili akiwamo aliyekuwa Katibu Mkuu, Kassim Dewji, Swedi Mkwabi, Mulamu, Ngh'ambi na Crescentius Magori.

Simba ilikubali pia kichapo kutoka kwa watani zao katika mechi ya marudiano ya Ligi Kuu Tanzania Bara, ikitolewa mapema katika mashindano ya Kombe la FA lakini ikimaliza msimu huu katika nafasi ya tatu nyuma ya mabingwa, Yanga na Azam FC.

Kwa matokeo hayo, msimu ujao katika mashindano yanayoandaliwa na kusimamiwa na Shirikisho la Soka Afrika, Simba itawakilisha nchi kwenye michuano ya Kombe la Shirikisho Afrika sambamba na Coastal Union ya jijini, Tanga.

Mabingwa wa Ligi Kuu Tanzania Bara, Yanga na Azam FC, wao watachuana katika mashindano ya Ligi ya Mabingwa Afrika.