Watumishi wadaiwa kutafuna mamilioni TASAF

By Shaban Njia , Nipashe Jumapili
Published at 01:49 PM Mar 24 2024
Fedha.
PICHA: MTANZANIA
Fedha.

BAADHI ya watumishi wa Halmashauri ya Msalala, Kahama mkoani Shinyanga, wanadaiwa kuhujumu zaidi ya Sh. milioni 39 walizotakiwa kuwapatia wanufaika wa Mfuko wa Maendeleo ya Jamii (TASAF).

Fedha hizo ni kupitia Mpango wa Kunusuru Kaya Masikini kutoka Kata 18 kwa kuwalipa wanufaika kipindi kimoja badala ya vipindi vitatu kama ulivyo utaratibu.

Watumishi hao wanadaiwa kutumia fursa ya uelewa mdogo wa wanufaika kwa kuwapa fedha za kipindi kimoja, hali iliyoibua malalamiko kwa baadhi yao kuambizana wamelipwa vipindi vyote vitatu.

Malalamiko hayo yaliibuliwa katika mkutano wa hadhara ulioitishwa na wananchi wa kata ya Isaka kujadili shughuli za kimaendeleo pamoja na kero zao uliomshirikisha mkurugenzi, viongozi wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) na Mbunge wa Jimbo hilo, Iddi Kassimu, ambaye walimtaka kuingilia kati ili fedha hizo zirejeshwe kwa wanufaika.

Mkazi wa Segese, Mussa Unyango, amesema walikuwa na vipindi vitatu hajawalipwa fedha za TASAF ambazo husaidia kukuza mitaji yao kwa wale wenye biashara ndogo pamoja na kilimo kwa kununua pembejeo lakini baadhi wamelipwa fedha zote na wengine wamelipwa kipindi kimoja tu.

“Sisi tunaomba mbunge uliingilie kati suala hili ili tufahamu tatizo ni nini baadhi yetu walipwe vipindi vitatu na sisi tunatoka kata za pembezoni tulipwe kipindi kimoja. Kama TASAF wameanza kutubagua tujue,” amesema.

Akijibu malalamiko hayo, Kaimu Mkurugenzi wa Halmashauri hiyo, Mfilingi Abdallah, amekiri baadhi ya watumishi kula fedha hizo kwa kutumia njia ya uelewa mdogo wa wanufaika  kujinufaisha na sasa wamewabana kuhakikisha fedha zinarejea.

Amesema kati ya Sh. milioni 39 zinazodaiwa kuliwa, tayari Sh. milioni 22 zimesharejeshwa na zilizobaki ni Sh. milioni 17.

Amesema fedha hizo ni miongoni mwa Sh. milioni 49 ambazo zilitokana na hoja za Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) kwa mwaka wa fedha uliopita na watumishi waliohusika katika ubadhirifu huo, wamesimamishwa kazi na taratibu zingine za kisheria na kiutumishi zinaendelea.

Mwenyekiti wa Halmashauri hiyo, Mibako Mabubu, amesema ili kuondoa malalamiko hayo walikubadiliana kupitia kamati ya fedha ambayo ilimwagiza Mkurugenzi wa Halmashauri,Hamisi Katimba, kutoa fedha zilizobaki kwenye mapato yao ya ndani na kuwalipa wanufaika, huku wakiendelea kuwashughulikia watumishi waliohusika.

Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Shinyanga, Mabala Mlolwa, ametoa siku saba kuhakikisha fedha hizo zinapatikana na kuwafikia walengwa wa TASAF ikiwa ni pamoja na kupata taarifa ya hatua zilizochukuliwa kwa wahusika waliokula fedha hizo kwa kuwa, wamefanya kosa kwa mujibu ya utumishi wa umma.

Mbunge Kassimu amesema hatakubali kuona wananchi wanapokonywa haki zao zinazotakiwa kupewa kisheria.

Amesema atahakikisha anakula sahani moja na wahusika hao na kuwataka wengine wenye tabia za namna hiyo kuacha mara moja, kwani fedha hizo zinatolewa kwa lengo la kumaliza umasikini na sio vinginevyo.